Sunday, July 31, 2011

Mashabiki wa bendi ya Extra Bongo wakiserebuka kwenye onyesho la vunja jungu, jijini Dar es Salaam.

Extra Bongo sasa kuwa na onyesho moja wakati huu wa mfungo wa Ramadhan.

Bendi ya Extra Bongo 'Wazee wa Kizigol', inatarajia kutumia kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili huku ikifanya onyesho moja kwa wiki.
Hayo yalisemwa na meneja wa bendi hiyo, Mujibu Hamis wakati akizungumzia kile ambacho kitafanywa na Extra Bongo wakati wote wa mfungo huo ambao ulianza juzi.
Alisema, ingawa bendi hiyo imekuwa ikiombwa kwenda mikoa mbalimbali kutoa burudani, wanamuziki wameona ni bora kwanza wakamilisha albamu hiyo ili wawe na nyimbo za kutosha katika maonyesho yao.
"Ndivyo tulivyoamua kwamba wakati wa Ramadhan tuwe na onyesho moja tu kwa wiki ili siku nyingine tuzitumie katika kukamilisha nyimbo za albamu ya pili lakini akija mtu kutukodi tukwenda kumfanyia kazi," alisema Mujibu.
Meneja huyo alifafanua kuwa hilo onyesho moja kwa wiki litakuwa linafanyika kila Jumamosi katika ukumbi wa Meeda club uliopo Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Alisema, Extra Bongo imekalimisha baadhi ya nyimbo za albamu ya  pili zikiwemo za 'Fisadi wa Mapenzi, 'Watu na Falsafa', 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Nguvu na Akili', 'Mtenda Akitendewa' na 'Msinitenge'.
"Kwa ujumla ni kwamba tunataka tukamilishe albamu ya pili wakati wa mfungo wa Ramadhan, ndio maana tukajiwekea ratiba hiyo ya kufanya onyesho moja kwa wiki huku tukiendelea kurekodi na kushuti video," alisema.
Extra Bongo ilianza kwa albamu ya 'Mjini Mipango' ikiwa na nyimbo za 'Laptop', 'First Lady', 'Maisha Taiti', 'Safari ya Maisha' na  Wema ambazo zimekuwa 'zikiporomoshwa' kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Aidha, bendi hiyo kwa sasa imekuwa ikifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani zikiwemo za 'Fadhila kwa Wazazi', 'Mwaka wa Tabu' na nyingine nyingi ambazo Ally Choki na Rogert Hegga waliwahi kutamba nazo.

Monday, July 25, 2011

Mnenguaji mpya wa bendi ya Extra Bongo, Aisha Madinda (wa pili kulia) akiwa pamoja na wanenguaji wenzake 'wakishambulia' jukwaa kwenye onyesho la bendi hiyo.

Baada ya Aisha Madinda, Extra Bongo yajiandaa kuongeza mwingine

Ikiwa ni siku chache tu baada ya kumchukua mnenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta, Aisha Madinda, uongozi wa bendi ya Extra Bongo umesema unajiandaa kuongeza mwanamuziki mwingine mpya atakayechukuliwa siku yoyote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki aliiambia SUGUTIRAHA kuwa iko mbioni kuendelea kujiimarisha kwa kuongeza mwanamuziki mwingine kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa kimuziki.
Choki alisema kuwa huenda mwanamuziki huyo mpya akatambulishwa kwenye maonyesho ya vunja jungu ambayo yatafanyika kwenye kumbi za burudani za jijini Dar es Salaam.
 "Tutakayemchukua atakuwa ni mwanamuziki wetu wa mwisho kuongezwa kwenye bendi ya Extra Bongo, lakini kwa sasa jina lake litaendelea kuwa siri li wabaya wetu wasije wakaingilia kati na kutuharibia," alisema.
Alisema, kitakachofanywa na Extra Bongo ni kuwashangaza wapenzi na wadau wa muziki wa dansi ni kumtambulisha mwanamuziki huyo kwenye maonyesho ya vunja jungu kama mambo yatakwenda kulingana na jinsi walivyopanga.
Alifafanua kuwa leo Jumatano bendi hiyo itaendelea na onyesho lake kama kawaida katika ukumbi wa Masai Bar na kufuatiwa na lingine kesho katika ukumbi wa Mzalendo Pub Makumbusho.
"Baada ya hapo yatafuatia maonyesho ya vunja jungu ambayo mwanamuziki wetu mpya anaweza kuwepo kuanzia Ijumaa katika ukumbi wa hoteli ya Vatican City, Sinza na kisha Jumamosi katika ukumbi wa Meeda," alisema.
Mkurugenzi huyo aliongeza kusema kuwa watakuwa na mwanamuziki wao huyo kwenye onyesho la Jumapili litakalofanyika kwa mara ya kwanza katika ukumbi wa Afri-Centre eneo la Msimbazi Ilala.
Extra Bongo ambayo inatamba na albamu ya kwanza ya 'Mjini Mipango', Extra Bongo pia inaandaa nyimbo za albamu ya pili ikiwa imekamilisha 'Mtenda Akitendewa', 'Watu na Falsafa',  'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema' na 'Msinitenge'.

Mwanamuziki mpya wa bendi ya Kalunde, Anania Ngoriga (kulia) akifanya vitu vyake na Bob Rudala kwenye onyesho la bendi hiyo.

Anania Ngoriga naye ajiunga na bendi ya Kalunde

Mwanamuziki wa siku nyingi Anania Ngoriga ambaye ni mlemavu asiyeona, amejiunga na bendi ya muziki wa dansi ya Kalunde yenye maskani yake Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Ngoriga alijiunga rasmi na Kalunde wiki iliyopita ambapo tayari ameshaanza kushiriki kwenye maonyesho ya bendi hiyo kwenye kumbi mbalimbali za burudani na kuonyesha makali yake.
Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo ndani ya Kalunde, kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala, alisema ana uhakika wa bendi yake kuingia kwenye muziki wa ushindani kwa vile inaundwa na wanamuziki wazoefu.
"Siyo kwamba ni wanamuziki wazoefu tu, kwa ujumla ni kwamba Kalundi inaundwa na wanamuziki wanaoujua muziki kwa hiyo tuna uhakika wa kupata soko la muziki la ndani na nje ya nchi," alisema Rudala.
Alisema kuwa karibu wanamuziki wote wa Kalunde wana uwezo wa kuimba na kupiga vyombo vya muziki na kwamba bendi zenye wanamuziki wa aina hiyo hapa nchini ni chache ikiwemo Kalunde.
"Mfano mzuri ni huyu Ngoriga ambaye anaimba na pia anajua kupiga gita la solo, rythm na bendi, hivyo tuna uhakika wa kufanya mambo makubwa kwenye muziki wa dansi," alisema.
Rudala alisema kuwa mwanamuziki huyo amejiunga na Kalunde wakati ikiwa kwenye maandalizi ya albamu mpya ikiwa imekamilisha nyimbo nne za 'Masumbuko', 'Sisee', 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini'.
Mbali na hilo, aliongeza kuwa Ngoriga amekuta waimbaji wawili wa bendi hiyo ambao ni Sarafina Mshindo na Mwapwani Yahaya wakiwa kwenye mashindano ya Bongo Star Search baada ya kufanikiwa kuingia 14 Bora.
"Furaha yetu imeongezeka zaidi, kwanza tulifurahi waimbaji wetu kuingia kwenye 14 Bora ya Bongo Star Search na sasa tumefurahi zaidi kwa kumpata mzoefu wa muziki wa dansi, Anania Ngoriga," alisema.
Naye Ngoriga mwenyewe alisema kuwa amejiunga na Kalunde akitokea katika bendi ya Karafuu ya visiwani Zanzibar ambayo alidumu nayo kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema, amejiunga na Kalunde kwa kutambua kuwa ni bendi yenye wanamuziki wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi ya muziki na kuongeza kuwa atashirikiana nao ili kuhakikisha kwamba inazidi kupiga hatua.

Mashabiki wa bendi ya Extra Bongo wakiwa wamembeba juu juu Aisha Madinda kwenye onyesho la bendi hiyo.

Friday, July 22, 2011

Aisha Madinda apagawisha wapenzi wa Extra Bongo, aonyesha kwamba yeye bado ni mkali katika kunengua.

Mnenguaji mpya wa bendi ya Extra Bongo 'Next Level', imesababisha wapenzi wa bendi hiyo kushindwa kujizuia na kuwafanya wainuke na kumbeba juu-juu kwenye onyesho lililofanyika katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Dar es Salaam.
Onyesho hilo lilikuwa ni mwendelezo wa maonyesho ya utambulisho wa mnenguaji huyo aliyejiunga na bendi hiyo akitokea Twanga Pepeta ambapo amekuwa akionyesho umahiri wake wa kusakata muziki wa dansi.
Utambulisho wake ulianza Jumatano ya Julai 20 katika ukumbi wa Masai uliopo Ilala na kisha kufuatiwa na mwingine katika yukumbi wa Mzalendo Pub uliosababisha mashabiki washindwe kujizuia na kumbeba juu kwa furaha.
Awali kabla ya tukio hilo, Aisha akiwa na wanenguaji wenzake walicheza shoo ya pamoja ambapo licha ya kutoonekana jukwaani kwa miezi mingi, alikuwa mwepesi, mwelevu na mjanja wa kwenda sambamba na wenzake.
Baada ya shoo ya pamoja aliachiwa nafasi yake kuamsha 'midadi' ya wapenzi wa Extra Bongo waliofurika kwenye ukumbi huo ambao 'walivamia' jukwaa na kumbeba juu kwa juu huku wakimtuza kuonyesha kuwa wameridhika na kiwango chake.
Kabla ya yote hayo, ilianza shoo kali ya wanenguaji wa wanne wa kiume walioshambulia jukwaa wakati kibao cha 'Mjini Mipango' kikipigwa, huku kikiendelea kupigwa ndipo Aisha alipopanda jukwaani kuonyesha uwezo wake.
Kama ilivyo kawaida, kabla ya mnenguaji huyo kupanda jukwaani, mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki alimwita Aisha ambapo alitumia dakika sita kucheza kabla ya wapenzi kuweweseka na kuvamia jukwaa na kumbeba juu-juu.
Baadaye wapenzi hao walimshusha ndipo aliendelea kuonyesha kuwa bado ana uwezo mkubwa wa kushambulia jukwaa kwa kiwango cha juu licha ya ukweli kwamba alikuwa nje ya jukwaa kwa kipindi kirefu akipigania afya yake.
Alipomaliza kazi yake, Aisha alijikuta akiondoka na kitita cha fedha alizotuzwa ingawa haikufahamika mara moja kwamba fedha zilikuwa ni kiasi gani.
Alipopewa nafasi ya kutoa maoni ya jinsi alivyopokelewa, Aisha alisema amefarijika kwa mwitikio wa mashabiki wengi waliojitokeza kwenye onyesho hilo na kwamba hakutegemea kupata mapokezi makubwa kwenye maonyesho mengine.

Thursday, July 21, 2011

Sehemu ya jengo la utawala la Chuo kipya cha Ualimu Mbezi cha Mbezi Kwa Yusuph jijini Dar es Salaam kinachotarajiwa kuanza rasmi Jumatatu ya Julai 25 mwaka huu.

Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Mbezi Teacher's Training College, David Msuya akiwa ofisini kwake, Mbezi Kwa Yusuph, jijini Dar es Salaam.

Chuo kipya cha Ualimu chaanzishwa Mbezi Kwa Yusuph, Dar es Salaam.

Chuo kipya cha Ualimu kimeanzishwa Mbezi Kwa Yusuph, jijini Dar es Salaam kinachojulikana kama Mbezi Teacher's Training College ambacho kinatarajia kuanza kupokea wanafunzi Julai 25 kwa ajili ya masomo.
Tayari baadhi ya wanafunzi wameshaanza kujisajili kwa ajili ya masomo yao chuoni hapo huku Mkuu wa chuo hicho, David Msuya akisema kuwa chuo hicho kina mandhari nzuri ya kuwavutia wanafunzi.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa chuo anasema kuwa kimesheheni kila kitu kuanzia maktaba, maabara, mabweni  na vitu vingine vinavyotakiwa katika vyuo vya ualimu hapa nchini.
"Pia tuna walimu wa kutosha wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kwenye kazi ya ufundishaji, hivyo nina uhakika wanafunzi watakaokuja kusoma hapa wataridhika na kile watakachokipata.

Tuesday, July 19, 2011

Mkurugenzi wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka akiwa ofisini kwake Buguruni Malapa, jijini Dar es Salaam.

waajiri wafanyakazi wa majumbani, watakiwa kuacha kuwaita watumishi hao kwa majina mabaya.

Watu wanaowaajiri wafanyakazi wa majumbani, wametakiwa kuacha kuwaita watumishi hao kwa majina mabaya, kwa madai kwamba kufanya hivyo ni kushusha hadhi na utu wao.
Hayo yalisemwa na wawezeshaji wa semina ya Waajiri Makini iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE linalohudumia Afya na Maendeleo ya Wanawake na watoto ambalo kifupi linajulikana kama kiota.
Pamoja na hayo, wametakiwa kuepuka kuwaajiri wafanyakazi wenye umri chini ya miaka 17 kutokana na ukweli kwamba ajira kwa watoto wadogo kosa kulingana na sheria za kimataifa kuhusu ajira za watoto.
Kwa mujibu wa Edda Kawala na Stella Mwambenja ambao wote wanatoka  KIWOHEDE, tabia ya waajiri kuwaita majina mabaya watumishi wao na kuwanyanyasa ama kuwabagua ni jambo baya kwani linashusha hadhi na utu wao.
Wawezeshaji hao walisema ni wajibu waajiri kuishi vizuri na watumishi wao na  kuwafanya kama sehemu ya familia zao badala ya kuwabagua na kunyanyapaa, kitu ambacho sio ubinadamu.

Wanenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta (kushoto) wakifanya vitu vyao huku wanamuziki wa Msondo Ngoma nao wakiwajibika jukwaani.

Twanga Pepeta na Msondo Ngoma kuchangia matibabu ya Gurumo.

Bendi za Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na Twanga Pepeta, zinatarajiwa kufanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za kusaidia matibabu ya mwanamuziki mkongwe, Muhidin Ngurumo.
Onyesho hilo litafanyika Jumamosi hii ya Julai 23 katika ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ndivyo mratibu wa Hassan Rehan ameiambia SUGUTIRAHA.blogspot.
Hassan alisema sehemu ya fedha zitakazopatikana kwenye onyesho hilo la pamoja zitakabidhiwa kwa mzee Ngurumo ama familia yake ili zitumike kwa ajili ya matibabu yake.
"Tuna uhakika kwamba wadau wa muziki wa dansi watakumbuka ambavyo mkongwe huyo wa muziki nchini alivyolazwa mara kadhaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," alisema Rehan.
Mratibu huyo alisema kuwa kutokana na Gurumo kuendelea kuugua, bendi za Twanga Pepeta na Msondo Ngoma zimeamua kufanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za matibabu kwa mzee huyo.
"Kwa ujumla ni kwamba maandalizi ya onyesho hilo yamekamilika ambapo kwa upande wa Twanga Pepeta itatumia nafasi hiyo kutambulisha nyimbo za albamu mpya inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu," alisema.
Alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Kauli', 'Kiapo cha Mapenzi', 'Umenivika Umasikini', 'Mtoto wa Mwisho', 'Dunia Daraja' na 'Penzi la Shemeji' utunzi wake Mwinjuma Muumin 'Kocha wa Dunia'.
Alifafanua kuwa kutokana na kuguswa na afya ya Gurumo, Twanga Pepeta ameamua kufanya onyesho hilo kwa vile  mchango wake ni mkubwa kwenye muziki wa dansi na ni mshauri wa karibu wa bendi ya Twanga.
Rehani amewaomba Watanzania na hasa wapenzi wa muziki wa dansi kujenga utamaduni wa kusaidiana kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kuchangia matibabu ya wanamuziki ambao kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi wamejikuta wakishindwa kukidhi mahitaji ya gharama za matibabu wanapoumwa.

Mshindi wa Kimwana wa Twanga 2011 aziba nafasi ya Aisha Madinda aliyejiunga na bendi ya Extra Bongo.

Bendi ya African Stars 'wanga Pepeta' imemchukua Mshindi wa shindano la 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011, Mary Khamis kuwa mnenguaji wa bendi hiyo.
Kwa mujibu wa Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya ASET inayomiliki bendi hiyo, kimwana huyo amechukuliwa ili kuziba nafasi ya Aisha Madinda aliyejiunga na Extra Bongo.
"Mpaka kufikia hatua ya kumchukua Mary ni baada ya kuvutiwa na kiwango chake cha uchezaji kwa kuwa alionyesha kipaji cha hali ya juu katika shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 na hatimaye kuibuka mshindi," alisema.
Asha alisema ana imani hapo baadaye kimwana huyo atakuwa mmoja wa wanenguaji mahiri hasa kwa kuzingatia kwamba ametingwa kwenye shindano la 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011' na kuwashinda wenzake tisa.
Alifafanua kuwa kwa sasa Twanga Pepeta ina wanenguaji wa kike tisa na wa kiume wanne aliowataja kwa majina ya  Abdillahi Zungu, Kassim Mohammed 'Super K', Bakari Kisongo 'Mandela' na Said Mtyanga.
Kwa upande wa wanenguaji wa kike aliwataja Fasha Sunday, Beatrice Mwangosi 'Baby Tall', Asha Said, Regina Filbert, Grace Kaswaka, Vicky Pandapanda, Lillian Tungaraza 'Internet', Sabrina Mathew na Maria Soloma.
Wakati huo huo, Asha alisema kuwa bendi yake kwa kushirikiana na Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' zitafanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za kusaidia matibabu ya mwanamuziki mkongwe, Muhidin Ngurumo.
Alisema onyesho hilo litafanyika kesho Jumamosi katika ukumbi wa Mango Garden Kinondoni ambapo pia atatambulishwa rasmi 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011' kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
"Twanga imeandaa onyesho hilo kwa kuguswa na afya ya Ngurumo ambaye mchango wake ni mkubwa kwenye  mwanamuziki wa dansi kwa miaka mingi na ni mshauri wa karibu wa bendi ya Twanga ," alisema Asha.
Mkurugenzi huyo alisema, kila mdau wa muziki hasa wa dansi anayefuatilia maendeleo ya muziki nchini atakumbuka jinsi mkongwe Ngurumo alivyowahi kulazwa mara mbili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na maradhi.

Mshindi wa shindano la 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011' Mary Khamis (katikati) akiwa na mshindi wa pili (kulia) Leila Mshana na mshindi wa tatu Hawa Miraji.

Ally Choki (wa pili kushoto) na baadhi ya wanenguaji wake wakinyanyuana mikono alipomtambulisha Aisha Madinda (kushoto) mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam. Kulia ni kiongozi msaidizi wa shoo, Otilia Boniface na kiongozi wa shoo, Super Nyamwela.

Monday, July 18, 2011

Ally Choki (wa pili kushoto) na baadhi ya wanenguaji wake wakinyanyua mikono alipomtambulisha Aisha Madinda (kushoto) mbele ya waandishi wa habari.Kulia ni kiongozi msaidizi wa shoo, Otilia Boniface na kiongozi wa shoo, Super Nyamwela.

Aisha Madinda aamua kutimkia Extra Bongo

Mnenguaji nyota wa bendi ya Twanga Pepeta, Aisha Madinda, amejiunga na bendi ya Extra Bongo 'Next Level' ambayo iko chini ya ukurugenzi wa Ally Choki.
Aisha alitambulishwa na Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo, Choki mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Makumbusho, jijini Dar es Salaam.
Katika utambulisho huo, Choki alisema kuwa ana uhakika mnenguaji huyo atatoa mchango mkubwa katika bendi yake, kwa madai kwamba ni mzoefu wa kazi na pia ana mashabiki wengi.
"Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa Aisha amechoka, lakini ukweli ni kwamba badio ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kama alivyo banzastone ambaye naye alianza kubezwa," alisema Choki.
Choki alisema kuwa mnenguaji huyo atatambulishwa rasmi Jumatano ya Julai 20 kwenye bendi hiyo katika onyesho litakalofanyika ndani ya ukumbi wa Masai uliopo Ilala.
Alifafanua kuwa utambulisho wa mnenguaji huyo utaendelea Ijumaa ya Julai 22 wakati Extra Bongo itakapokuwa mjini Musoma mkoani Mara ikifanya vitu vyake katika ukumbi wa Magereza.
Aliongeza kuwa Jumamosi Extra Bongo itakuwa jijini Mwanza na kisha Jumapili itamalizia burudani na kumtambulisha mnenguaji huyo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria mjini Geita.
'Nina uhakika nguvu imeongezeka kwenye shoo ya Extra Bongo hasa kwa kuzingatia kwamba uwezo wa Aisha ninaujua kutokana na ukweli kwamba nilishafanya naye kazi kwa muda mrefu," alisema.
Kwa upande wake Aisha alisema kuwa ameachana na Twanga Pepeta baada ya kuona watu wake ambao alikuwa akifanya nao kazi kwa karibu wamehamia Extra Bongo.
"Kule kwa sasa hakuna vitu kama ambavyo viko Extra Bongo, hivyo ninawaomba mashabiki wangu waje huku Extra Bongo wanione nikiendeleza makamuzi kwani bado niko fiti katika muziki," alisema Aisha.
Alisema kuwa wiki moja iliyopita alikuwa kwenye mazoezi makali chini ya kiongozi wa shoo wa Extra Bongo, Super Nyamwela ili kuzijua staili za bendi hiyo na kwamba sasa yuko tayari kupanda jukwaani na kufanya vitu vyake.

Mratibu wa mradi wa watumishi wa nyumbani kanda ya Afrika, Vicky Kanyoka akizungumzia upitishaji wa mkataba unaowatambua watumishi wa majumbani.

Friday, July 15, 2011

Waajiri wa wafanyakazi wa majumbani ambao ni wakorofi kukumbana na rungu

Upitishaji wa mkataba wa kimataifa wa 189 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO ni kama ni 'rungu' kwa waajiri walio na wafanyakazi wa majumbani watakaokiuka sheria na mikataba ya kazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta nyingine.
Mkataba huo wa kuwatambua wafanyakazi hao ulipitishwa Juni 16 mwaka huu katika mkutano wa 100 wa ILO uliofanyika nchini Uswisi na siku moja kabla ya kupitishwa, Rais Jakaya Kikwete alihutubia mkutano huo kuuridhia.
Akizungumzia hatua hiyo, Mratibu wa Shirika la Wafanyakazi wa Majumbani kwa Kanda ya Afrika, IUF, Bi. Vicky Kanyoka, alisema kuridhiwa kwa mkataba huo kumetoa fursa na nafuu kwa watumishi hao wa majumbani.
Kanyoka, alisema kulingana na mkataba huo, wafanyakazi wa majumbani watatambuliwa kama wafanyakazi wengine, kulindwa na kupewa haki zao ikiwemo kusainishwa mikataba na makubaliano kabla ya kuanza kazi kwa muajiriwa.
Mratibu huyo alisema kitu cha muhimu baada ya kupitishwa kwa mkataba huo ni serikali ya Tanzania na wananchi wake kuutekeleza kwa vitendo ili wafanyakazi hao wanajivunie kazi yao tofauti na siku za nyuma walipokuwa wakijificha.
"Kwa hakika kupitishwa kwa mkataba huo wa 189 ni kama rungu kwa wafanyakazi wa majumbani, watawabana waajiri wao, ambao kwa miaka mingi waliwabagua, kuwanyanyasa na kuwadharau wakiwachukulia kama 'vijakazi'," alisema.
Aliwataka watumishi hao kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mkataba huo kwa kutokubali kuajiriwa kabla ya kuingia mkataba na kuridhia haki zao stahiki katika ajira ili inapotokea tatizo mbele ya safari iwe rahisi kusaidiwa.
Aliwataka pia waajiri kuridhia na kuutekeleza mkataba huo kwa kuamini watumishi hao ni kama sehemu ya familia zao na hivyo kuwapa huduma na stahiki zote kama mishahara kulingana na kima wanachokubaliana na kwa muda muafaka.
Mratibu huyo alisema mkataba huo ulipitishwa kwa kupigiwa kura 396 za ndio huku kura 16 zikiukataa miongoni mwa nchi zilizougomea ikiwa ni taifa la Uingereza, huku mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania na yale ya Amerika Kusini na Kaskazini yakiongoza kwa kuupitisha.

Wednesday, July 13, 2011

Wanenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta wakionyesha umahiri wao wa kucheza muziki kwenye onyesho la bendi hiyo katika ukumbi wa Mango Garden.

Twanga Pepeta sasa ina kazi ya kuangusha moja moja

Baada ya kukamilisha utunzi wa nyimbo za albamu ya 11, bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta International', imeanza kazi ya kurekodi nyimbo hizo hatua hadi zote zinakamilisha kurekodiwa.
Mkurugenzi wa kampuni ya ASET inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka amesema kuwa albamu hiyo ambayo haijapewa jina inaundwa na nyimbo sita.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni 'Dunia Daraja', 'Mapenzi Hayana Kiapo','Kauli', 'Mtoto wa Mwisho', 'Penzi la Shemeji' na 'Talaka Harusini' ambazo sasa zinapigwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
"Wanamuziki wameshaanza kuingia studio ili kurekodi nyimbo hizi , lakini katika hizo upo mmoja ambao tulishaurekodi na Bozi Boziana," alisema Asha.
Aliutaja wimbo huo kuwa ni 'Mapenzi Hayana Kiapo' ambao mkongwe huyo wa muziki wa dansi barani Afrika ameshiriki kikamilifu na waimbaji wake wa wawili wa kike aliotua nao hapa nchini hivi karibuni.
"Tutaendelea kuangusha moja moja studio ili kuhakikisha kwamba zote zinarekodiwa, yote haya ni maandalizi ya uzinduzi wa albamu yetu ambayo tumepanga kuizindua kabla ya kumalizika mwaka huu," alisema.
Bendi hiyo ambayo sasa inajiita 'Wazee wa Kisigino', imekuwa na utaratibu wa kuzindua albamu kila mwaka ambapo sasa inajiandaa kufanya uzinduzi huo wa albamu ya 11.
Twanga Pepeta pia imekuwa ikifanya maonyesho matano kwa wiki ikianzia Jumatano ambapo huwa katika ukumbi wa Billicanas  na kufuatiwa na lingine Alhamisi katika ukumbi wa Sun Cirro.
Kwa siku ya Ijumaa bendi hiyo imekuwa ikizunguka kwenye kumbi mbalimbali kulingana na maombi ya mashabiki wake na kisha Jumamosi katika ukumbi wao wa nyumbani wa Mango Garden Kinondoni.
Jumapili mchana Twanga Pepeta hufanya vitu vyake kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni kabla ya kumalizia wikiendi kwa kufanya onyesho usiku katika ukumbi wa TCC Club Chang'ombe.

Mashujaa Musica yahangaikia mbili ili kukamilisha albamu ya pili.

Huku ikiendelea kukamilisha albamu ya pili, bendi ya Mashujaa Musica iko mbioni kumalizia nyimbo mbili za mwisho ili kukamilisha albamu ya pili ambayo inaandaliwa na bendi hiyo inayojiita 'Wana Posoposo'.
Rais wa bendi hiyo Jado Field Force alizitaja nyimbo hizo zinazofanyiwa na mazoezi na wanamuziki wa Mashujaa Musica kuwa ni 'Shukrani' na 'Mahakama ya Mapenzi'.
Wakati bendi hiyo ikiendelea na mazoezi ya kumalizia nyimbo hizo mbili, Jado alisema tayari wamesharekodi nyingine tatu ambazo amezitaja kwa majina ya 'Hukumu ya Mnafiki', 'Uchungu wa Moyo' na 'Lucia'.
"Kwa ujumla ni kwamba tuna nyimbo za kutosha albamu nzima lakini tunarekodi tatu na sasa tunaendelea kufanyia mazoezi nyingine mbili za mwisho huku zikiwepo zilizokamilika lakini hazijarekodiwa," alisema Jado.
Aliutaja wimbo wa 'Ulishawahi Kwenda kwa Mkweo' kwamba ni mojawapo ya zilie zilizokamilika lakini hazijarekodiwa ambapo utarekodiwa pamoja na hizo za  'Shukrani' na 'Mahakama ya Mapenzi' zinazoendelea kufanyiwa mazoezi.
Alisema ana uhakika kufikia mwishoni mwa mwezi huu Mashujaa Musica itakuwa imekamilisha nyimbo zote za albamu ya pili na kwamba itakuwa imebaki kazi ya kurekodi na kushuti video.
Rais huyo alisema kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa bendi hiyo imekuwa ikitamba na albamu ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na kufafanua kuwa ni wakati muafaka kuandaa albamu nyingine ili isaidie kuitambulisha zaidi bendi hiyo.
"Tunaendelea kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya kuteka soko la muziki wa dansi hapa nchini ndio tunaandaa nyimb kali zaidi ambazo tuna uhakika kwamba zitawavutia zaidi mashabiki wa muziki wa dansi," alisema.

Baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Mashujaa Musica wakiwa kazini.

mbunga wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere akiwahutubia wakazi wa jimbo hilo hivi karibuni.

Baadhi ya wakazi wa jimbo la Musoma Mjini nao wataka posho ziondolewe

Baadhi ya wakazi wa Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara, wameungana na Chadema na kuitaka serikali kuondoa posho za wabunge, watumishi wake na kuachana vikao visivyo na tija ili fedha zielekezwe katika matatizo ya msingi.
Vicent Nyerere ambaye ni mbunge wa jimbo hilo kwa tikati ya Chadema ndiye aliyesema hayo akiwakariri wakazi wa jimbo lake waliimpa ujumbe huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mara Sekondari.
Nyerere alisema wananchi wakazi hao walimwambia hayo kwenye mkutano wake alioutisha mjini humo ili wamweleze kero  zinazowabili na yeye mwenyewe (Nyerere) kuwaleleza utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.
Wakazi wa jimbo langu wanataka fedha zielekezwe kwenye huduma za kijamii na kwa upande wa elimu na afya ambako ndiko kwenye matatizo mengi ambayo hadi sasa hajapatiwa ufumbuzi," alisema Nyerere.
Mbali na hilo, alisema kuwa wakazi wa jimbo lake pia walimuomba apeleke ujumbe kwa serikali kwamba  wanataka kujua kwa nini mafuta yanaendelea kupanda bei wakati serikali ilishatangaza kuwa kufikia Julai mosi yangeshuka bei.
Aidha, alisema kuwa katika mkutano huo aliagiza wafanyabiashara wote ambao wamepewa vibali vya kununua mahidi kwenye ghala la taifa Shinyanga ili kukabiliana na njaa jimboni humo wayapeleke haraka.
Alisema wapo baadhi yao wameingia mitini huku mmoja wao akiwa amepewa kibali vya kuleta tani 100 za mahindi ambapo amemwagiza eleta mahindi ama arudishe kibali kabla ya kukumbana na mkono wa sheria.
"Jimbo langu lina kata 13 kama wafanyabiashara waliopewa vibali wangefikisha mahindi kwa wakati, makali ya njaa yangepungua, lakini ujanja huu unaofanywa na baadhi ya wafanyabishara unachangia kuwepo kwa njaa," alisema.
Nyerere pia alikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuangalia kama fedha zilizotolewa zikitumika ilivyotakiwa na ameona hakuna ufisadi uliofanyika na kwamba kila kitu kilifanyika vizuri.
Mbunge huyo aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara, madaraja na ukarabati wa madawati ya shule za msingi na kufunga madampo likiwemo la soko la Nyakato mjini humo.
Katika hatua nyingine, Nyerere alisema kuwa ujenzi wa maabara ya kisasa itakayotumiwa na shule tano za sekondari za kata zilizojengwa kwenye kata moja jimboni humo, unatarajia kuanza hivi karibuni.
Alisema ujenzi huo utaanza kufuatia mfuko wa jimbo kuwa na jumla ya shilingi milioni 34 na kwamba awali mfuko huo ulikuwa na shilingi milioni 17 ambapo zimeongezeka nyingine milioni 17 na kufikia milioni 34.
Alisema kuwa fedha hizo zitatosha kujenga jengo la maabara, kuweka meza na viti na kwamba ataendelea kusubiri nyingine ambazo zitatumika kununulia vifaa vya maabara ili wanafunzi waanze kuitumia.

Mpiga kinanda wa bendi ya Extra Bongo, Pablo Mashine akiwa kazini kwenye onyesho la bendi hiyo katika ukumbi wa Mzalendo Pub.

Extra Bongo kufanya usajili wa dirisha dogo'

Bendi ya Extra Bongo 'Next Level' inatarajia kutumia kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili kukamilisha kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili huku ikifanya onyesho moja kwa wiki.
Kiongozi wa bendi hiyo Rogert Hegga ndiye aliyeliambia gazeti la NIPASHE wakati akizungumzia mikakati iliopo mbele ya Extra Bongo mara baada ya kuanza kwa mwezi huo Mtukufu.
Mbali na hilo, kiongozi huyo alisema Extra Bongo inatarajia kutumia kipindi hicho kuongeza 'kifaa' kimoja ambacho kitatambulishwa mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kukichukua.
"Tutakachokifanya ni usajili wa dirisha dogo kama ilivyo kwenye timu za soka, tunaongeza mwanamuziki mmoja tu na siwezi kumtaja kama ni mwimbaji mpiga chombo ila itajulikana wakati muafaka ukifika," alisema.
Alisema kuwa bendi hiyo sasa inajivunia mafanikio ambayo imeanza kuyapata ikiwa ni pamoja na kukubalika kwa mashabiki wa dansi wa ndani na nje ya jijini la Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alisema kuwa wiki chache zilizopita bendi hiyo ilifanya ziara kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro kwa ajili ya kujitambulisha kwa mashabiki wa dansi na kupokelewa kwa kishindo.
"Mashabiki wetu walijitokeza kwa wingi kutuunga mkono kwenye maonyesho yote ambayo tumefanya kwenye mikoa hiyo na ndivyo ilivyo hata jijini Dar es Salaam ambapo pia wamekuwa wakizidi kujitokeza kwa wingi," alisema Hegga.
Hegga alisema kuwa kwa sasa Extra Bongo imekalimisha nyimbo mpya za 'Watu na Falsafa', 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Nguvu na Akili', 'Mtenda Akitendewa' na 'Msinitenge' ambazo ni maandalizi ya albamu ya pili.
Aidha katika kutoa burudani, Hegga alisema kuwa leo Jumamosi bendi hiyo itafanya vitu vya ndani ya ukumbi wa Zakhem Mbagala na kesho itamalizia katika ukumbi wa mpya wa Chiluba uliopo Mabibo Mwisho.

Monday, July 11, 2011

Karibuni SUGUTIRAHA.blogspot,utawezajipatia habari mahiri za michezo na burudani na matukio mengine ya kijamii. Unakaribishwa kuleta matangazo ya aina mbalimbali, utahudumiwa kwa gharama nafuu kabisa…

Bendi ya FM Academia yafiwa na Meneja Mauzo wake, Bonny.

Bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia imepata pigo kwa kufiwa na Meneja Mauzo wake, Bonny Kasyanju aliyefariki dunia usiku wa kuamia leo Julai 11 baada ya kuugua kwa muda wa mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa Msemaji wa bendi hiyo, Kelvin Mkinga, Bonny alikukuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ini na figo
ambapo alilazwa katika hospitali ya Lugalo,  jijini Dar es Salaam hadi mauti ilipomkuta.
"Bado mipango ya mazishi inaendelea kufanyika, baada kukamilika tutatoa taarifa zaidi, lakini ni kwamba kwa sasa tuna msiba wa kufiwa na Meneja Mauzo wetu Bonny," alisema Mkinga.
Hata hivyo, Msemaji huyo hakufafanua zaidi kama bendi hiyo itasimamisha maonyesho ili kuomboleza msiba kwa madai kwamba hadi ratiba ya mazishi itakapotolewa na familia ya marehemu.

Andrew Sekidia akipiga kinanda huku rais wa bendi ya Akudo, Christian Bella akishuhudia.

Mpiga kinanda Andrew Sekidia kuungana na Akudo mwezi huu.

Mpiga kinanda wa bendi ya Akudo Impact 'Vijana wa Masauti', Andrew Sekidia ambaye kwa sasa yuko Umangani akifanya shughuli za muziki huko, anatarajia kurudi kwenye bendi hiyo mwishoni mwa mwezi huu.
Meneja Uhusiano Msaidizi wa bendi hiyo, Ramadhan Pesambili, alisema, Sekidia aliaga na kwenda Oman kufanya kazi ya muziki kwa mkataba wa miezi mitatu ambao sasa unakaribia kumalizika.
"Sekidia atarudi kundini mwishoni mwa mwezi huu kwani tayari tumeshawasiliana naye akathibitisha kuwa kufikia Julai mwishoni atakuwa amesharudi ili kuendelea na kazi kwenye bendi yake ya Akudo," alisema Pesambili.
Pesambili alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa kwamba wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa mwanamuziki huyo ameitosa Akudo na kukimbilia nje ya nchi kufanya kazi ya muziki wa dansi.
"Huyo ni mwanamuziki wetu aliondoka kwa kuaga uongozi wa bendi na tumemuomba kwamba arudi na kinanda kingine ili tuwe na viwili, kwa hiyo taarifa kwamba ameacha bendi hazina ukweli wowote," alisema.
Meneja Uhusiano huyo Msaidizi aliongeza kusema kuwa Sekidia ndiye anayesubuiriwa ili kupiga kinanda kwenye nyimbo za albamu ya pili ya 'History no Change' ambazo bendi hiyo imezikamilisha.
Alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Ubinafsi', 'Umefulia', 'Pongezi kwa Wanandoa', 'Umejificha Wapi' ambapo Sekidia ataingia studio kwa ajili ya kucharaza kinanda.
Bendi hiyo inayoongozwa na Christian Bella imekuwa ikitamba na albamu ya kwanza ya 'Impact' ambayo ilichangia kuipandisha chati kwa nyimbo kali ukiwemo wa 'Yako Wapi Mapenzi'.

Sunday, July 10, 2011

Mzee Kassim Mapili (kushoto) ambaye amejiunga na bendi ya Rufita Connection akiwa na Mrisho Mpoto.

Mkongwe wa muziki wa dansi, mzee Kassim Mapili atua Rufita Connection

Mpiga solo na mwanamuziki wa siku nyingi, mzee Kassim Mapili amejiunga na bendi mpya ya muziki wa dansi ya Rufita Connection yenye maskani yake Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam, imeelezwa.
Hayo yameelezwa na rais wa bendi hiyo, Chai Jaba alipokuwa akizungumza na gazeti la NIPASHE kufuatia hatua ya mkongwe huyo wa muziki kujiunga na Rufita ambayo inatumia mtindo wa 'Shika Hapa Acha Hapa'.
"Utu uzima ni dawa ndio maana sisi Rufita Connection tumemchukua mtu mzima mzee Mapili ambaye sasa anasaidiana na Abdalah Kibugila katika upigaji wa gita la solo," alisema Chai Jaba.
Alisema ana uhakika msaada ama ushauri wake utakuwa mkubwa kwenye bendi hiyo mpya ambayo inaundwa na sehemu kubwa ya wanamuziki vijana na hivyo kuifanya izidi kupiga hatua.
Rais huyo alisema kuwa mzee Mapili amejiunga na bendi hiyo ikiwa ni wiki chache tangu imchukue Kibugila aliyeziba nafasi ya Seleman Shaibu Mumba aliyechukuliwa na bendi ya Twanga Pepeta.
"Pia mzee mapili amejiunga na kukuta tumeshakamilisha nyimbo za albamu ya kwanza ambazo ni Mapenzi Yanaua, Nilinde Nikulinde, Anasa, Shida ya Mapenzi, Usia, Acha Pupa, Mkosi Gani na Mazi.
Kuhusu mikakati zaidi ya bendi hiyo, Chai Jaba inajiandaa kumalizia kazi ya kurekodi nyimbo zote na kisha itafuata kazi ya kushuti video ya nyimbo hizo kabla ya kuanza utaratibu wa uzinduzi wa albamu.
Mbali na mikakati hiyo, alisema bendi hiyo inajiandaa kuleta wanenguaji wapya wanne kutoka Congo (DR) watakaokuja kuungana na wenzao waliopo ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji wa jukwaa.

Kiongozi mpya wa bendi ya Kalunde, Bob Rudala, akiimba kwenye onyesho la bendi hiyo katika ukumbi wa Joevic , Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Bob Rudala awa bosi wa bendi ya Kalunde

Mwimbaji wa siku nyingi wa muziki wa dansi, Bob Rudala, aliyejiunga na bendi ya Kalunde hivi karibuni akitokea katika bendi ya InAfrika, ameteuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa bendi hiyo, Doborah Nyangi, uongozi wa juu ndio umemteua Rudala kushika nafasi hiyo ambayo awali ilikuwa ikikaimiwa na mwimbaji Junior Grengo.
Deborah alisema, Rudala aliteuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo tangu wiki iliyopita baada ya uongozi wa juu wa Kalunde kukutana na kuamua kwamba ndiye apewe jukumu la kuiongoza bendi.
"Tunaamini kwamba ana uwezo mkubwa wa kuongoza, ndio maana mabosi wetu wamekaa na kuamua kumteuwa kuwa kiongozi wa bendi yetu kwani ni mwanamuziki mzoefu ambaye amefanya hii kwa muda mrefu," alisema Deborah.
Alifafanua kwa muda mrefu bendi hiyo haikuwa na kiongozi ambapo Junior Grengo alikuwa akiishikilia kwa muda ambapo sasa nafasi hiyo amepewa Rudala huku Deo Mwanambilimbi akiendelea kuwa rais wa bendi.
Aidha, alisema kuwa Rudala amechukuwa nafasi ya uongozi wa bendi wakati ikiendelea na mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili ikiwa imekamilisha nne za 'Masumbuko', 'Sisee' na 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini'.
"Tunafanya mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili huku tufanya maonyesho kama kawaida kwa siku za Jumatano na Ijumaa ambapo huwa tunatoa burudani katika ukumbi wa Triniti uliopo Oysterbay," alisema.
Meneja huyo aliongeza kuwa siku ya Jumamosi Kalunde imekuwa ikitoa burudani katika ukumbi wa Joevic Mbezi Beach na kisha Jumapili huwa ndani ya ukumbi wa Giraffe Hotel ambao pia upo Mbezi Beach.
Wakati huo huo Meneja hjuyo alisema, bendi hiyo inayotumia mtindo wa 'Lekendepuke', inajivunia wanenguaji wake wawili, Queen Vero na Aminatha Othman, kwa madai kwamba wanajua kazi na wanajituma vilivyo wawapo jukwaani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa wingi wa wanenguaji kwenye bendi kama yao haina umuhimu wowote hasa kwa kuzingatia kwamba huwa inapiga muziki kwenye kumbi tulivu ambazo hazihjitaji kuwa na kundi kubwa la wanenguaji.

Thursday, July 7, 2011

Jijini la Dar es Salaam bila uchafu haiwezekani?

Kalunde yajivunia wanenguaji wake

Bendi ya Kalunde 'Wana Lekendepuke', imesema kuwa inajivunia wanenguaji wake wawili, Queen Vero na Aminatha Othman, kwa madai kwamba wanajua kazi na pia wanajituma vilivyo wawapo jukwaani
Meneja wa bendi hiyo, Doborah Nyangi ndiye amesema hayo na kuongeza kuwa wanenguaji hao wanatosha na kwamba Kalunde haina mpango wa kuongeza wengine zaidi ya hao wawili.
"Tuna wanenguaji makini wanaoshirikiana kwa karibu katika kazi, wanapendana na wanajua kufanya kazi ya muziki, hivyo  hatuoni sababu yoyopte ya kuongeza wengine, hawa wanatutosha na tunajivuna kuwa nao," alisema Deborah.
Alisema kwa wingi wa wanenguaji kwenye bendi kama yao haina umuhimu wowote hasa kwa kuzingatia kwamba huwa inapiga muziki kwenye kumbi tulivu ambazo hazihjitaji kuwa na kundi kubwa la wanenguaji.
"Wingi wa wanenguaji nao nio tatizo, kwani uzoefu unaonyesha kwamba wakiwa wengi hawawezi kufanya kazi kwa kushirikiana, kila mmoja atataka kujiona kuwa ni bora kuliko mwingine," alisema.
Alisema bendi hiyo sasa inajiandaa kuwa ya kimataifa, hivyo idadi tya wanamuziki waliopo inatosha na kwamba inaweza kuongeza wengine pale inapobidi lakini sio kwa upande wa wanenguaji.
Bendi hiyo imekuwa kambini kwa zaidi ya miezi miwili sasa huku ikiandaa nyimbo mpya na nyingine za kukopi huku ikiendelea na maonyesho kama kawaida kwenye ambazo imekuwa ikitoa burudani.
Nyimbo mpya zilizokambilishwa kwenye kambi ya bendi hiyo ni  'Masumbuko', 'Sisee' na 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini' ambazo baadhi yake zimeanza kusikika kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Miongoni mwa kumbi ambazo Kalunde imekuwa ikitoa burudani ni Triniti ambako bendi hiyo hufanya vitu vyake kila Jumatano na Ijumaa kisha Jumamosi huwa Joevic na kumalizia wikiendi katika ukumbi wa Giraffe Ocean View, Mbezi Beach.

Wanenguaji wa bendi ya Kalunde, Aminatha Othman (kushoto) na Queen Vero wakifanya vitu vyao.

Rapa nyota wa bendi ya Mashujaa Musica, Sauti ya Radi, akifanya makamuzi ya nguvu.

Rapa wa Mashujaa Musica atoa wimbo wa 'Mahakama ya Mapenzi'

RAPA wa bendi ya Mashujaa Musica, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', amesema kuwa amekamilisha kibao kiitwacho  'Mahakama ya Mapenzi' ambacho kimekamilisha albamu ya pili inayoandaliwa na bendi hiyo.
Sauti ya Radi ambaye ni Makamu wa Rais wa bendi hiyo, alisema kuwa Mashujaa Musica imekuwa kwenye maandalizi ya albamu ya pili ambapo imekamilisha kwa wimbo wake wa 'Mahakama ya Mapenzi'.
Mbali na wimbo huo nina rapu nyingi ikiwemo ya Kikombe cha Babu Loliondo ambayo kwa kweli ni moto wa kuotea mbali na imekuwa ikipendwa na mashabiki wengi wa bendi yetu ya Mashujaa Musica," alisema.
Alisema kuwa wimbo wake umeunganishwa na nyingine za 'Lucia', 'Uchungu wa Moyo', 'Ulishawahi Kwenda kwa Mkweo', 'Hukumu ya Mnafiki' na 'Shukrani' ambazo sasa zimekuwa zikipigwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Alifafanua kuwa bendi hiyo inaandaa albamu ya pili huku ikiendelea kuuza ile ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na  kuongeza kuwa kamilika kwa nyimbo mpya hakuna maana kwamba bendi hiyo itazindua albamu ya pili mapema.
Mwaka jana bendi hiyo ilizindua albamu hiyo ya 'Safari Yenye Vikwazo' ambayo hadi sasa imeendelea kutambulisha kwenye kumbi mbalimbali za ndani na nje ya jijini Dar es Salaam.
Bendi hiyo pia imekuwa ikifanya maonyesho matano kwa wiki ikianzia Jumatano hadi Jumapili kwa ajili ya kutamhulisha albamu hiyo na kujiongezea mashabiki zaidi wanaofika kuishuhudia.
Alisema kuwa kila Jumatano bendi hiyo imekuwa ikipatikana katika ukumbi wa Max Bar na kisha kuzunguka katika kumbi mbalimbali ukiwemo wa Mashujaa Night Park, Vingunguti na Bwalo Maofisa wa Magereza Ukonga.

Waimbaji wa bendi ya Kalunde, Mwapwani Yahaya (kulia) na Sarafina Mshindo wakiimba kwenye onyesho la bendi hiyo, jijini Dar es Salaam.

Waimbaji wawili wa bendi ya Kalunde waingia Bongo Star Search

Waimbaji wawili wa kike wa bendi ya Kalunde, Mwapwani Yahaya na Sarafina Mshindo, wamechukuliwa kwa muda kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Bongo Star Search.
Meneja wa Kalunde, Deborah Nyangi ambaye ni mwimbaji pekee wa kike aliyebaki kwa sasa katika bendi hiyo,  ameliambia gazeti la NIPASHE kuwa uongozi umewaruhusu waimbaji hao kushiriki mashindano hayo.
"Kila wanapokuwa na nafasi wamekuwa wakienda kama kawaida kwenye maonyesho kama kawaida huku wakiendelea na mashindano hayo ambayo yaliwafanya wajulikane hadi tukawachukua mwaka 2009," alisema.
Alisema kuwa waimbaji hao wamechukuliwa kwenye mashindano hayo wakati bendi yao ikiwa kwenye maandalizi ya nyimbo za albamu ya pili ambazo wameshiriki kikamilifu.
Alisema kuwa hatua ya uongozi wa bendi kuwaruhusu wanamuziki hao kwenda kwenye mashindano hayo inalenga kutambua mchango wa kampuni Benchmark Production ambayo iliibua vipaji vyao hadi wakachukuliwa na Kalunde.
"Bila Benchmark sisi Kalunde tusingewajua  Mwapwani na Sarafina, hivyo tunaheshimu sana mchango wa kampuni hiyo kwenye sanaa na hasa ya muziki wa dansi na kizazi kipya," alisema Deborah.
Kalunde ambayo hivi karibu ilipata mwanamuziki mpya Bob Rudala, kwa zaido ya mwezi mmoja saa iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili na tayari imekamilisha nyimbo nne mpya.
Nyimbo hizo ni 'Masumbuko', 'Sisee', 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini' ambao umetungwa na Bob Rudala aliyejiunga na bendi hiyo akitokea katika kundi la InAfrika ambayo imekuwa ikipiga muziki kwenye nchi mbalimbali.
Huku ikiendelea kuandaa nyimbo mpya, bendi hiyo pia imekuwa ikitoa burudani kila Ijumaa katika ukumbi wa Triniti Oysterbay, Jumamosi huwa Joevic Pub Mbezi Beach na Jumapili katika ukumbi wa Giraffe Hotel Mbezi Beach.

Huduma ya upimaji afya bure iliyoendeshwa na Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai yawavutia wengi wakiwemo ambao sio waumini wa kanisa hilo.

Hivi karibuni Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai, jijini Dar es Salaam, kupitia Idara ya Afya, Kaya na Familia liliendesha zoezi la kupima afya bure ambapo zaidi ya watu 1,000 walipata huduma hiyo.
Mchungaji wa kanisa hilo, Daniel Msholla, alisema huduma za kiafya ni moja kati ya huduma za muhimu zinazotolewa na kanisa lake likiamini ili kufikia malengo ni muhimu kwa mwanadamu kujua hali yake kiafya na kupata matibabu.
Alisema kanisa lake limekuwa likiendesha na kutoa huduma hiyo kila mwaka likitambua kuwa wananchi wengi wakiwemo waumini wake hawana uwezo wa kulipia gharama za vipimo mbalimbali vya afya.
Baadhi ya magonjwa yaliyochunguzwa ni kisukari, VVU, viungo, akili, matiti, macho na magonjwa mengine ya akina mama ambapo zoezi hilo lilishirikisha pia wakazi wanaoshi maeneo ya karibu na kanisa hilo.
Mmoja wa madaktari walioshiriki kwenye zoezi hilo, Dk. Herman Elihaki wa kituo cha Afya Magomeni alisema hatua ya kanisa ilisaidia watu wengi kufika na kuchunguzwa afya zao hasa kitengo cha macho alichokuwa akishughulikia.
Naye Dk.Benedetha Shirio kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema zoezi hilo lina maana kubwa kwa watu wa kawaida ambao wengi wao wanaugua maradhi mbalimbali lakini hawajitambui kwa kuwa hawana uwezo wa kugharamia vipimo.
Baadhi ya watu waliopata huduma hiyo ambao sio waumini wa kanisa hilo, waliushukuru uongozi wa kanisa kuomba zoezi hilo lizidi kuimarishwa ili kuendelea kutoa huduma hiyo kila mwaka kwa ufanisi zaidi.
Kwa sasa kanisa hilo linaendelea na mahubiri ya wiki tatu kwenye viwanja vya Biafra  Kinondoni ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakifika kupata neno la Mungu liletalo wokovu.
Mahubiri hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano wa Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai na Kanisa la Wasabato Manzese, sasa yameingia wiki ya pili tangu yaanze ambapo watu wamekuwa wakijitoa kwa wingi ili kumtumikia Mungu.

Mmoja wa madatari walioshiriki zoezi la kuwapima watu afya bure lililoendeshwa na Kanisa la Wasabato, Magomeni Mwembechai, Dk. Phoibe Koshuma (kushoto) akimpima mtu urefu kabla ya kumpa huduma nyingine.

Baadhi ya wanenguaji wa bendi ya FM Academia wakiwajibika jukwaani.

Wazee wa Ngwasuma waja na Usiku wa Tende, Haluwa

BENDI ya FM Academia kwa kushirikiana na kampuni ya Afrika Kabisa Entertainment (ake), wanatarajia kufanya maalum lililopewa jina la Usiku wa wa Tende na Haluwa linalolenga kutambulisha nyimbo mpya za albamu ya pili.
Kwa mujibu wa msemaji wa bendi hiyo, Kelvin Mkinga, onyesho hilo litafanyika Ijumaa Julai 8 katika ukumbi wa burudani wa Vaticna City Hotel Sinza, jijini Dar es Salaam.
Katika onyesho hilo, bendi hiyo inatarajia kutambulisha baadhi ya nyimbo zikiwemo za Fataki, Chuki ya Nini na Ndoa Bandia ambazo zimekuwa zikisikika kwenye maonyesho mbalimbali ya bendi hiyo inayojiita Wazee wa Ngwasuma.
"Kampuni ya Afrika Kabisa Entertainment (ake) imetusaidia kuandaa onyesho hili ambalo limepewa jina la Usiku wa Tende Haluwa ambalo litafanyika katika ukumbi wa Vatican Sinza," alisema Mkinga.
FM Academia ni moja ya bendi zenye mashabiki wengi ambayo kila Jumamosi hutoa burudani katika ukumbi wa Kijiji cha Makumbusho na kisha Jumapili humalizia wikiendi kwenye bonanza katika ukumbi wa New Msasani Club.
Bendi hiyo imeendelea kujiimarisha ambapo sasa ina waimbaji wawili wa kike ambao ni Joyce Musiba 'Mpongo Love' na Sarah Andembwisye Mwangyombo 'Belabeloo' ambao wanashirikiana kwa karibu kufanya kazi kwenye bendi hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Elimu, Kassim Majaliwa akimkabidhi mifuko ya unga wa sembe diwani wa kata ya Chinongwe, Phabian Nguli, alipotembelea jimboni mwake.

Wednesday, July 6, 2011

Mbunge Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa aendelea kuwasaidia wananchi wa jimbo lake.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Chinongwe jimbo la Ruangwa mkoani Lindi ambao hivi karibuni walioathiriwa na mvua, wamepata msaada wa unga na mabati ili visaidie kuendesha maisha yao ya kila siku
Msaada huo ulitolewa na mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa.
Kila mara mbunge huyo amekuwa akifika jimboni mwake humo kuwajulia hali wapiga kura wake na kuwatatulia kero mbalimbali zinazowakabili kulingana na hali inavyoruhusu.
Jimbo la Ruangwa lina kata 21 ambapo mbunge huyo ameshatembelea kata zaidi ya 10 kwa ajili ya kuwashukuru wapiga kura wake na pia kutatua baadhi ya kero zinazowakabili.
Yeye binafsi anasema, kuwa karibu na wananchi ndio njia pekee ya kujua matatizo na changamoto zinazowakabili na pia njia mojawapo ambayo itasaidia kubuni na kuibua mkakati wa kuwaletea maendeleo.
"Nitaendelea kuwatembelea wapiga kura wangu kwa sababu nimeahidi kuwatumikia kwa nafasi hii ya ubunge, hivyo ninawajibika kuwatembelea na kuwajulia hali na hata kusaidina nao kutatua kero mbalimbali
zinazowakabili," alisema Majaliwa.

Diwani wa kata Ndugumbi, Charles Mgonja akizungumza na wajumbe wa nyumba kumi

Wajumbe wa nyumba 10 CCM nao wanataka kulipwa posho!

WAKATI sakata la kutaka posho za wabunge ziondolewe likiendelea kuwa gumzo miongoni mwa wananchi, wajumbe wa nyumba kumi wa CCM nao wameibuka na kutaka wawe walipwa posho hizo ili wanufaike nazo.
Kwa sasa sakata hilo limemalizwa bungeni baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutamka bungeni kuwa zitaendelea kutolewa licha ya baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani kutaka ziondelewe.
Hatua hiyo ya wabunge wa upinzani kutaka posho za kukaa bungeni ziondolewe na serikali ya kuamua ziendelee kuwepo imezua gmijadala miingi mitaani na kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni.
Sehemu kubwa ya wakazi wa Dar es salaam waliozungumza na gazeti hili walionyesha kutoridhishwa na kuendelea kuwepo kwa posho hizo huku wakitaka fedha zielekezwe kwenye matatizo yanayowakabili Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, wajumbe wa nyumba kumi wa CCM nao wameibuka na kutaka walipwe posho kama ambavyo madiwani na wabunge wanavyopata wanapokuwa kwenye vikao vyao.
Waliodai posho hizo ni wajumbe wa nyumba kumi wa kata ya Ndugumbi, jijini Dar es Salaam walipokuwa kwenye kikao kilichoitikishwa na diwani wa kata hiyo, Charles Mgonja ili kujadili utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Diwani huyo alielezea utekezaji wa ilani ya chama hicho ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwenye maeneo kadhaa ya kata yake na kwamba serikali inaendelea kutekeleza ilani ya CCM.
Baada ya hapo ndipo wajumbe wakapewa nafasi ya kuuliza maswali ama kutoa dukuduku zao ambapo walianza kuelezea uchafuzi wa mazingira na vibanda vya video ambavyo vindaiwa kuwaharibu watoto.
Aliyeanza kuchangia ni mjumbe wa shina namba 15 Kagera Mikoroshini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Mwenjala aliyedai kuwa kwenye eneo lake mkandarasi wa kuzoa taka amekuwa hafiki kwa wakati kuzoa taka.
Alisema hali hiyo inasababisha wananchi kulazimika kutupa taka kwenye mitaro hasa baada ya kuona mkandarasi haji kwa wakati ili kuzichukua na kuzipeleka kwenye dampo.
Wakati mjumbe huyo akisema hayo, mwingine aliyejitambulisha kwa jina la MagdalenaNguyeje wa shina namba 24, Kagera Kisiwani, alilalamikia vibanda vya video vilivyoko mitaani ambavyo sasa vinachangia kuwaharibu watoto.
Baada ya mjumbe huyo, aliibuka mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Mhangia wa shina namba 31, Kagera Kisiwani na kudai kuwa umefika wakati sasa wajumbe wa nyumba kumi nao wapete posho.
"Na sisi sasa tunastahili kupata posho kama ilivyo kwenu madiwani na wabunge, hivyo tunakuomba mheshimiwa diwani utusaidia kwa hilo, siyo posho ziishie huko juu tu, zishuke hadi kwetu huku," alisema Mhangia.
Ombi la mjumbe huyu liliunmgwa mkono na mwingine aliyejitambulishwa kwa jina la Hellena Muya wa shina la 10, Kagera Kisiwani aliyesema kuwa wao pia wanafanya kubwa, hivyo wanastahili kupata posho.
Akijibu maombi hayo, diwani huyo alisema suala la posho kiachiwe chama ngazi ya taifa kwa vile kinalijua na kwamba yeye hana uwezo wa kulitokea maamuzi na pia kwenye manispaa hakuna posho za wajumbe wa nyumba kumi.
Kuhusu kuwepo kwa vibanda vya video vinavyowaharibu watoto, aliwaomba wajumbe hao kushirikiana na viongozi wao wa serikali za mitaa ili kukomesha hali hiyo na kuhakikisha watoto wanakwenda shule badala ya kuishia vibandani.
"Suala na mkandarasi wa kuzoa taka kuchelewa nitafuatilia, lakini pia wananchi wahimizwe kulipia fedha za uzoaji taka na wala wasiendelee kutupa taka kwenye mitaro, huo ni uchafuzi wa mazingira," alisema Mgonja.

Bob Rudala akiimba kwenye moja ya maonyesho ya bendi ya Kalunde.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere akiwapungia mkono wananchi wa jimbo lake.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere aja na mbinu za kuboresha elimu jimboni mwake

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara, Vicent Nyerere (Chadema), amesema kuwa anajiandaa kujenga maabara ya kisasa itakayotumiwa na shule tano za sekondari za kata zilizojengwa kwenye kata moja.
Nyerere ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Jimbo, alisema hayo alipokuwa akizungumzia mkakati wa kuboresha elimu kwenye jimbo lake.
"Uchache wa maeneo ya kujenga shule, ilibidi shule za sekondari za Bweri, Nyabisarye, Iringo, Nyamatare na Kamunyonge zijengwe kwenye kata moja ya Bweri," Nyerere.
Mbunge huyo alisema kuwa kwa hali hiyo inabidi ijengwe maabara moja kubwa na ya kisasa kwenye shule ya sekondari ya Bweri ambayo itakuwa inatumiwa na wanafunzi wa shule hizo tano.
Alisema maabara hiyo itajengwa kwa fedha za mfuko wa jimbo ambapo aliongeza kuwa hadi sasa mfuko huo una  shilingi milioni 17 na kwamba ana uhakika kwa ushirikiano na Manispaa mkakati huo utafanikiwa.
Alifafanua kuwa anaendelea kuwasiliana na wataalam wakiwemo wahandishi wa Manispaa ya Mji wa Musoma kuona uwezekano wa kuangalia eneo na kisha kuandaa michoro ya jengo la maabara hiyo.
"Hiin pia haizuii kila shule kuwa na maabara yake ila nitakachokufanya ni kujenga maabara kubwa ambayo itakuwa na vifaa vyote kwa manufaa ya wanafunzi wa shule hizo tano zilizongwa kwenye kata moja," alisema.
Alisema, atafanya kila liwezekanalo kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa ya Mji wa Musoma ili kuhakikisha kwamba kwa mwaka mmoja ama miwili maabara iwe imekamilika na kuanza kazi.
"Nimesema tutajenga maabara ya kisasa nikiwa na maana itakuwa pia na chumba cha kompyuta zilizounganishwa na mtandao ili kuwasaidia wanafunzi kupata masomo kirahisi kwa njia ya mtandao," alisema.
Mbali na hilo, mbunge huyo alibainisha kuwa ubora wa maabara hiyo pia utaongezewa sehemu ambayo itatumika kufugia wanyama wadogo wakiwemo vyura na panya kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Aidha, aliwaomba wadau wa elimu wamuunge mkono katika juhudi zake hizo za kuboresha elimu jimboni mwake na hasa kampuni ya simu kutoa modem ili kupata mtandao mara baada ya maabara hiyo kuanza kazi.
"Moja vipaumbele vyangu wakati wa kampeni ilikuwa ni kuboresha elimu, hivyo ninaanzia kwenye maabara na kisha yatafuata maeneo mengine kulingana mfuko wa jimbo utakavyoruhusu," alisema.

Dotinata ambaye amepata mkataba wa kuuza kazi za wasanii wa filamu nchini Burundi

Dotinata kuuza kazi za wasanii wa filamu nchini Burundi

Dotinata aula nchini Burundi

MSANII  wa siku nyingi wa fani ya maigizo na filamu, Husna Posh 'Dotinata', amepeta mkataba nchini Burundi ambao unamruhusu kuuza kazi za wasanii mbalimbali wa filamu wa hapa Tanzania.
Akizungumza na gazeti la NIPASHE, jijini Dar es Salaam, msanii huyo alisema kuwa aliingia mkataba huo mwezi uliopita na kampuni ya Burundi Intertainment Association ya nchini humo.
"Ni mkataba endelevu ambao niliingia na kampuni mwezi Juni ambapo wateja wa nchi za Congo DR, Rwanda na Uganda watakuwa wanafika Bujumbura kununua kazi za wasanii wa filamu wa Tanzania," alisema.
Alifafanua kuwa yeye ndiye atakuwa ananunua filamu za wasanii wa hapa nchini na kuzipeleka Bujmbura ili zikauzwe huko, kwa madai kwamba filamu za Tanzania zina soko kubwa nchini Burundi na zile za jirani na nchi hiyo.
"Nilianza kwa kuleta wasanii watatu wa Burundi ambao ni Shanel, Excellent na Olga, walikuja kushiriki kwenye filamu yangu ya nne ya Chupa Nyeusi na sasa wamerudi kwao," alisema.
Aliwataja baadhi ya wasanii wa hapa nchini ambao wameshiriki kwenye filamu hiyo kuwa ni Irene Uyowa, Tino Muya, Patcho Mwamba, Riama na wengine wenye makubwa katika fani hiyo.
Alisema huo ulikuwa ni mwanzo wa kuanzisha urafiki ambapo yeye (Dotinata) alikwenda nchini Burundi na kupata mkataba wa kuuza kazi za wasanii filamu nchini humo na kwamba atahakikisha Tanzania inajulikana kwa fani hiyo.
Mbali na filamu ya 'Chupa Nyeusi', Dotinata alizitaja nyingine ambazo alishakamilisha kuwa ni 'Ndani ya Gunia', 'Sekeseke', 'Hila', Ulimwengu wa Wafu na nyingine ya sita ambayo bado haijapewa jina.

Askari polisi, waandishi wa habari, viongozi wa AJAAT na waendesha semina kutoka Marie Stopes wakiwa katika picha ya pamoja

Sera ya Ukimwi Mahali pa kazi yafanya watumishi wengi kuwa wazi

Sera ya Ukimwi Mahali ya pa Kazi imechangia watumishi wengi kuwa wazi mara wanapotambua kuwa wameathirika kwa ugonjwa huo hatari na hivyo kuwafanya wafuate maelekezo ya jinsi ya kuishi kwa matumain kwa kutumia dawa za kurefusha maisha.
Hayo yaliwekwa wazi hivi karibuni kwenye semina iliyowashirikisha askari polisi, waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiratibiwa na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi nchini AJAAT.
Semina hiyo iliendeshwa na Mkuu wa Mawasiliano wa Marie Stopes, Johnbosco Baso kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na kufanyika ukumbi wa Wanyama Hotel, Sinza jijini Dar es Salaam.

Nani kuwa mshindi wa Kimwana wa Twanga Pepeta 2011?

BAADA ya zaidi ya miaka mitatu, shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta limerudi tena ambapo sasa vimwana 10 waliofanikiwa kuingia kqwenye fainali ya kinyang'anyiro hicho watapanda jukwaani.
Mpambano huo utafanyika Ijumaa Julai 8 katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam ambapo vimwana 10 wapatanda jukwaani kila mmoja akitahidi kila linalowezekana ili ashinde.
Kwa mara ya kwanza shindano kama hilo lilifnyika mwaka 2006 ambapo mshindi alikuwa ni Lulu Semagongo ambaye ni maarufu kama 'Aunt Lulu' na kujishindia gari dogo.
Mwaka uliofuata wa 2007 lilifanyika shindano la pili ambalo mshindi wake alikuwa ni Halima Haroun ambaye naye alijinyakulia gari dogo na tangu mwaka huo halijafanyika tena shindano lingine hadi mwaka huu wa 2011.
Shindano la mwaka huu lina mabadiliko katika zawadi ambapo mshindi atazawadiwa duka la vipodozi lenye thamani ya shilingi milioni tano ambalo limelipiwa kodi ya mwaka mzima.
Waandaaji wa shindano hilo wamesema kuwa wamefanya mabadiliko hayo katika zawadi kwa kuzingatia umuhimu wa kumwendeleza mshindi ili aweze kujiajiri mwenyewe kwa biashara ya duka.
"Zawadi ya duka inaweza kumfanya kimwana akaliendesha vizuri, mwishowe likamletea mafanikio katika maisha, cha msingi ni kuzingatia mbinu za uendeshaji wa biashara," alisema mratibu wa shindano hilo.
Mratibu huyo Maimatha Jesse alisema kuwa vimwana wote katika kambi ya mazoezi walipata pia elimu ya biashara na ujasiriamali, hivyo ana uhakika mshindi wa shindano hilo ataweza kumudu kulitunza duka hilo atakalojishindia.
Mshindi wa pili anatarajia kupata kitita cha shilingi 500,000 wakati mshindi wa tatu atapata 300,000 ambapo washiriki wengine watapewa 100,000 kila mmoja kama kifuta jasho.

Vimwana kumi wa Twanga 2011 ambao watachuana vikali kwenye shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 wakiwa katika pozi.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere (katikati) akiwajulia hali wagonjwa hospitalini

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini atembelea wagonjwa hospitalini

Moja ya majukumbu ya mbunge ni kutembelea wananchi wake wakati wa shida na hata wa raha kama ambavyo amekuwa akifanya mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, mkoani Mara, Vicent Nyerere awapo jimboni mwake ambapo pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya jimbo hilo, amekuwa akitembea kwenye hospitali ili kuwajulia hali wagonjwa.
Yeye mwenyewe anasema kuwa siyo hospitali tu bali hutembelea pia kwenye magereza ili kuwajulia hali wafungwa na mahabusu na kuwasaidia kwa chochote pale inapowezekana, kwa kuwa wao pia ni binadamu wana matatizo yanaowakabili huko magerezani.

Mkurugenzi wa kampuni ya Papa-zi, Zakaria Hans Poppe akizungumzia mikakati ya kuibua vipaji vya wasanii wa filamu

Papa-zi yaja kuokoa vipaji vya wasanii wa filamu nchini

Papa-zi yaja kuokoa vipaji vya wasanii wa filamu nchini

BAADA ya kimya cha muda mrefu, hatimaye wadau wa sanaa wameanza kuchukua hatua za kusaidia kuibua na kukuza vipaji vya wasanii wachanga katika uigizaji ili kusaidia jitihada wanachofanya katika kujiendeleza kisanii.
Baadhi ya wadau hao ni kampuni ya Papa-zi ambayo imengaza mkakati kabambe wa kusaidia wasanii chipukizi jinsi ya kufuatilia hisia zao kisanii na kurekodi kazi zao na mwisho wa siku kusambaza ili kuwahakikishia soko.
Tayari kampuni hiyo imejipanga na kuweka wazi mikakati yake inayolenga kusimamia kazi zote za wasanii wachanga na hata wenye majina ili kila mmoja anufaike kupitia jasho lake.
Ili kuhakikisha kwamba kampuni hii inatimiza malengo yake, tayari imeshafanya kongamano kubwa kwa kushirikisha wadau wa filamu na kuelezea bayana kile ambacho inapanga kufanya katika fani ya filamu.
Katika kongamano hilo pia lilihamasisha wasanii waliokata tamaa ili warejee kwenye ulingo wa sanaa ili wapige kazi ya filamu kwa ajili ya kuelimisha, kuburudisha na kufundisha jamii kwa njia hiyo ya sanaa.
Kongamano hilo pia liliibuka na mawazo mapya ya kubadilisha taswira ya filamu nchini baada ya kuzoeleka kwa majina ya wasanii wakubwa huku wale wanaochipukia wakiendelea kusota bila kutambulika.
Meneja masoko wa kampuni hiyo, Issa Kipemba alisema Papa-zi imekuja kwa sura nyingine inayolenga kuwasaidia zaidi wasanii tangu wachanga na wale wenye majina makubwa.
“Kila kukicha katika filamu hakuna jipya, utaona wasanii ni wale wale tuliozoea kuwaona au kuona kazi zao, hali inayosababisha mawazo yao kuwa ni yaleyale, maeneo ya kuigiza ni yaleyale, na zaidi ya hapo utaona wazi kwamba tunaiga zaidi,” anasema Kipemba.
Mbali na hilo anasema kampuni yake inakuja na mabadiliko ikiamini kwamba kuna wasanii zaidi ya yeye (Kipemba) na pia wapo wasambazaji wa kazi zaidi ya watu wenye asili ya Kiasia wanaofanyakazi kazi hiyo kwa kiwango kikubwa sasa.
Anasema kuwepo kwa wasambazaji wachache kumechangia wasanii wa vijijini, wilayani na hata mikoani wenye vipaji tofauti kukosa soko kwa vile imezoeleka kwamba inapotoka filamu mpya, msambazaji anahoji juu ya msanii aliyeshiriki.
***
Kama filamu ikikosa msanii mwenye jina utakuta inanunuliwa kwa bei ndogo hali ambayo inachangia kuua vipaji vya wasanii ambavyo sasa kampuni ya Papa-zi imebaini hilo na imeamua kujitosa kuviokoa kwa kusambaza kazi zao.
“Kwa mfano inatokea mtu unatumia zaidi ya Sh. Milioni 5 kuandaa filamu, halafu msambazaji anahoji kama msanii fulani yumo au hayumo, na kama hayumo basi anasema atanunua kwa chini ya Sh. Milioni 2 au 3. Utabaini hizo ni dharau, ukiritimba ambao kampuni ya Papa-zi imepania kuufuta kabisa,” anasema.
Ili kufanikiasha malengo Papa-zi itafanya utafiti zaidi ili filamu zitakazochezwa na wasanii watakaowaibua na hata wenye majina, zisambazwe kwa ubora wa kazi na sio umaarufu wa jina ambao wengi kuiga filamu kutoka India au Nigeria.
Papa-zi inasema, hata wasanii wenye majina wameanza kudharauliwa na wasambazaji na wanyonyaji wengine wa kazi za wasanii na kwamba zipo filamu hazijamaliza mwezi tangu zitoke, lakini video zake zinauzwa kwa Sh 1,000 barabarani.
Kutokana na hali hiyo, kampuni ya Papa-zi imeazimia kufanya kila njia ili kuhakikisha kwamba wasanii waliokata tamaa wanaendelea na kazi hiyo bila kuzibiwa riziki na wale wanaojiona kama bila wao filamu Tanzania haiwezekani.

Dk. Musika Kandole (nyuma) akifundisha baadhi ya wanafunzi katika chuo cha KAM

Sehemu ya jengo la utawala la Chuo cha KAM kilichopo Kimara-Mavurunza

Chuo cha KAM kinavyojizatiti kuzalisha wataalam ktk sekta ya afya

Chuo cha Afya cha KAM kilichopo Kimara Mavurunza, jijini Dar es Salaam ambacho sasa kimesajiliwa na NACTE kwa kumbukumbu Na NACTE/BA/436/605/vol.xvi/98, kinatarajiwa kupata wanafunzi 30 ifikapo Septemba mwaka huu.
Mwenyekiti wa chuo hicho, Dk. Kandole Musika alisema kuwa kwa sasa kina wanafunzi 80 na kwamba kufikia wakati huo wa mwezi Septemba idadi ya wanafunzi wanaohitajika itakuwa imetimia.
"Chuo kinatarajia kuchukuwa wanafunzi 300, lakini kwa sasa wameanza 80 wakati taratibu nyingine zikiendelea hadi kufikia Septemba ambapo wataongezeka wengine zaidi," alisema.
Alisema kuwa masomo yanayotolewa chuoni hapo kwa sasa fani za wataalam wa Maabara yaani Medical Laboratory na Utabibu (Clinical Medicine).
"Baada ya chuo kutoa fani hizo kwa muda, baadaye kitaanza kujikita pia katika ufundishaji wa taaluma ya uuzaji na utoaji dawa (famasia) na wataalam wauguzi (Nursey)," alisema.
Aliongeza kusema kuwa ni imani yake kwamba baada ya miaka miwili kitaanza kutoa mchango kwa serikali kwa kupunguza tatizo la uhaba wa wataalam wa afya katika fani za maabara na utabibu.
Aidha, alisema KAM imefanikiwa kujenga madarasa nane, maabara kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo chuoni hapo  pamoja na mabweni 15 yenye uwezo wa kulaza wanafunzi nane kila moja.
"KAM College of Health Sciences ambacho kilianza kupokea wanafunzi Machi mwaka huu, kimethibitishwa rasmi Mei 19' 2011 kina uhakika wa kutoa wataalam wa afya miaka michache ijayo," alisema.

Baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Kalunde wakiwa mazoezini

Tuesday, July 5, 2011

Choki na baadhi ya wanamuziki wake wakisakata muziki

Bendi ya Extra Bongo 'Next Level' inatarajia kutumia kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili kukamilisha kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki mara baada ya kumaliza ziara ya siku tatu ya utambulisho wa nyimbo mpya na wanamuziki wapya mkoani Morogoro.
Ziara hiyo ilifanyika wiki iliyopita baada ya kumaliza ile ya mikoa ya Lindi na Mtwara iliyofanyika hivi karibuni kwa mafanikio makubwa kutokana na kupata mashabiki wengi waliohudhuria maonyesho ya bendi hiyo.
"Tumefanikiwa kujitambulisha kwa kushindo kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro na sasa tunajiandaa kutumia kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili ya kukamilisha albamu yetu," alisema Choki.
Choki alisema kuwa kwa sasa Extra Bongo ina nyimbo mpya za Watu na Falsafa, Fisadi wa Mapenzi, Neema, Nguvu na Akili na Msinitenge ambazo husikika kwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema ana uhakika kwamba kipindi chote cha Ramadhan kitatosha bendi hiyo kukamilisha kila kitu na hatimaye kuibuka kwa kishindo ikiwa na vitu vipya.
Mbali na hilo, Choki alisema kuwa katika mkakati ya kujiimarisha zaidi, bendi hiyo imepata gari dogo aina Hiace kwa  usafiri ambalo litakuwa linatumiwa na wanamuziki wake kwenda kwenye maonyesho na kurudi nyumbani.
"Tumeanza na gari hili dogo lakini kadri mambo yanavyokwenda ndivyo tutaangalia uwezekano wa kununua kubwa zaidi ambalo tutakuwa tunalitumia kwa safari za maonyesho kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini,"alisema.
Aidha katika kutoa burudani, leo Jumatano bendi hiyo inapatikana katika ukumbi wa Equator Grill, Mtoni kwa Aziz , kesho Alhamisi itakuwa katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Makumbusho.
Maonyesho hayo yatafuatiwa na lingine la Jumamosi katika ukumbi wa Dolphin, Kimara na kumalizia wikiendi Jumapili kwa kutoa burudani katika ukumbi wa Stereo uliopo Kinondoni.

Bendi ya Mashujaa Musica yapata wanamuziki wapya

Bendi ya Mashujaa Musica ambayo sasa inaendelea kukamilisha albamu ya pili, imeongeza wanamuziki wawili kundini ili kuendelea kuimarisha safu yake ya upigaji vyombo.
Kwa mujibu wa rais wa bendi hiyo, Jado Field Force, wanamuziki hao ambao walijiunga na Mashujaa Musica wiki iliyopita ni Kassim Hamis anayepiga gita la besi na Tatoo ambaye anapiga drums.
Jado alisema kuwa mpiga besi huyo ametokea bendi ya Rufita Connection yenye maskani yake Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam wakati mpiga drums amechukuliwa toka bendi mpya ya Ngoma Musica.
Rais huyo alisema awali bendi hiyo haikuwa na mpango wa kuongeza wanamuziki wapya kwenye bendi hiyo, lakini hata hivyo alifafanua kuwa sasa hali inawaruhusu kujiimarisha zaidi.
"Mwanzoni mwa mwaka huu tuliongeza wanamuziki na wanenguaji tukasema kwamba tumefunga milango ya kuchukua wanamuziki wapya, lakini imebidi tuongeze hawa wawili kwa sababu hali inaruhusu," alisema.
Alisema, bendi hiyo imeongeza wanamuziki wapya wakati ikiwa imekamilisha nyimbo za albamu ya pili za 'Lucia', 'Uchungu wa Moyo', 'Ulishawahi Kwenda kwa Mkweo', 'Hukumu ya Mnafiki', 'Shukrani' na 'Mahakama ya Mapenzi'.
Aliongeza kuwa mwaka huu ni Mashujaa Musica kuwa matawi ya juu kwa madai kwamba wamejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kujiimarisha kila idara kwa kupata wanamuziki wa kutosha wanaojua kazi ya muziki.
"Mwaka jana tulizindua albamu ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' ambayo hadi sasa imeendelea kuwepo sokoni wakati sisi tukiwa kwenye maandalizi ya albamu ya pili," alisema Jado.

Monday, July 4, 2011

sera ya Ukimwi Mahali pa kazi yafanya watumishi wengi kuwa wazi.

Sera ya Ukimwi Mahali ya pa Kazi imechangia watumishi wengi kuwa wazi mara wanapotambua kuwa wameathirika kwa ugonjwa huo hatari na hivyo kuwafanya wafuate maelekezo ya jinsi ya kuishi kwa matumain kwa kutumia dawa za kurefusha maisha.
Hayo yaliwekwa wazi hivi karibuni kwenye semina iliyowashirikisha askari polisi, waandishi wa habarim, viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi nchini AJAAT na wadau wa afya ya jamii.

Friday, July 1, 2011

Bob Rudala aipa Kalunde kibao cha Ulinipendea Nini

Mwezi mmoja baada ya kujiunga na bendi ya Kalunde, mwimbaji wa siku nyingi, Bob Rudala amegfyatia kibao cha 'Ulinipendea Nini' ambacho sasa kinafanyiwa mazoezi na wanamuziki wa bendi hiyo.
Kiongozi wa bendi hiyo Junior Grengo aliliambia gazeti la NIPASHE jana kuwa kibao hicho kitakuwa ni cha nne kukamilishwa na bendi hiyo ambayo iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili.
"Tulianza kukamilisha nyimbo tatu za 'Masumbuko', 'Sisee' na 'Fungua' ambazo tumekuwa tukizipiga kwenye maonyesho yetu ya kila mwisho wa wiki na sasa tunamalizia huu wa Rudala," alisema Grengo.
Alisema, kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa bendi hiyo imekuwa kambini ikiandaa nyimbo za albamu ya pili ikiendelea na maonyesho ya mwisho wa wiki katika kumbi mbalimbali za burudani ambapo sasa ina nyimbo nne.
"Rudala amejiunga na bendi yetu akiwa na wimbo wa Ulinipendea Nini ambao sasa uko hatua za mwisho kukamilika, huenda wiki ijayo ukaanza kusikika kwenye maonyesho yetu," alisema.
Alifafanua kuwa bendi hiyo imelazimika kuweka kambi ya mazoezi huku ikiendelea na maonyesho ya mwisho wa wiki ili isipoteze wapenzi na mashabiki wake ambao wamezoea kuishuhudia ikiwaburudisha.
Alisema kuwa kila Ijumaa kama leo imekuwa ikitoa burudani katika ukumbi wa Triniti uliyopo Oysterbay na kisha Jumamosi wamekuwa wakifanya vitu vyoa katika ukumbi wa Joevic, Mbezi Beach.
Mbali na maonyesho, alisema kuwa Jumapili hufanya bonanza ndani ya ukumbi wa Girraffe Oceanic View uliyopo Mbezi Beach ambapo siku zilizobaki huwa kambini kwa ajili ya mazoezi ya nyimbo mpya.
Aidha, hatua ya kumchukua Bob Rudala kutoka bendi ya InAfrika imekuwa ikielezwa kuwa inalenga kuifanya Kalunde ijulikane kitaifa na kimataifa kwa vile ana uzoefu wa kufanya kazi ndani na nje ya nchi.