Thursday, July 7, 2011

Huduma ya upimaji afya bure iliyoendeshwa na Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai yawavutia wengi wakiwemo ambao sio waumini wa kanisa hilo.

Hivi karibuni Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai, jijini Dar es Salaam, kupitia Idara ya Afya, Kaya na Familia liliendesha zoezi la kupima afya bure ambapo zaidi ya watu 1,000 walipata huduma hiyo.
Mchungaji wa kanisa hilo, Daniel Msholla, alisema huduma za kiafya ni moja kati ya huduma za muhimu zinazotolewa na kanisa lake likiamini ili kufikia malengo ni muhimu kwa mwanadamu kujua hali yake kiafya na kupata matibabu.
Alisema kanisa lake limekuwa likiendesha na kutoa huduma hiyo kila mwaka likitambua kuwa wananchi wengi wakiwemo waumini wake hawana uwezo wa kulipia gharama za vipimo mbalimbali vya afya.
Baadhi ya magonjwa yaliyochunguzwa ni kisukari, VVU, viungo, akili, matiti, macho na magonjwa mengine ya akina mama ambapo zoezi hilo lilishirikisha pia wakazi wanaoshi maeneo ya karibu na kanisa hilo.
Mmoja wa madaktari walioshiriki kwenye zoezi hilo, Dk. Herman Elihaki wa kituo cha Afya Magomeni alisema hatua ya kanisa ilisaidia watu wengi kufika na kuchunguzwa afya zao hasa kitengo cha macho alichokuwa akishughulikia.
Naye Dk.Benedetha Shirio kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema zoezi hilo lina maana kubwa kwa watu wa kawaida ambao wengi wao wanaugua maradhi mbalimbali lakini hawajitambui kwa kuwa hawana uwezo wa kugharamia vipimo.
Baadhi ya watu waliopata huduma hiyo ambao sio waumini wa kanisa hilo, waliushukuru uongozi wa kanisa kuomba zoezi hilo lizidi kuimarishwa ili kuendelea kutoa huduma hiyo kila mwaka kwa ufanisi zaidi.
Kwa sasa kanisa hilo linaendelea na mahubiri ya wiki tatu kwenye viwanja vya Biafra  Kinondoni ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakifika kupata neno la Mungu liletalo wokovu.
Mahubiri hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano wa Kanisa la Wasabato Magomeni Mwembechai na Kanisa la Wasabato Manzese, sasa yameingia wiki ya pili tangu yaanze ambapo watu wamekuwa wakijitoa kwa wingi ili kumtumikia Mungu.

No comments:

Post a Comment