Sunday, July 10, 2011

Mkongwe wa muziki wa dansi, mzee Kassim Mapili atua Rufita Connection

Mpiga solo na mwanamuziki wa siku nyingi, mzee Kassim Mapili amejiunga na bendi mpya ya muziki wa dansi ya Rufita Connection yenye maskani yake Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam, imeelezwa.
Hayo yameelezwa na rais wa bendi hiyo, Chai Jaba alipokuwa akizungumza na gazeti la NIPASHE kufuatia hatua ya mkongwe huyo wa muziki kujiunga na Rufita ambayo inatumia mtindo wa 'Shika Hapa Acha Hapa'.
"Utu uzima ni dawa ndio maana sisi Rufita Connection tumemchukua mtu mzima mzee Mapili ambaye sasa anasaidiana na Abdalah Kibugila katika upigaji wa gita la solo," alisema Chai Jaba.
Alisema ana uhakika msaada ama ushauri wake utakuwa mkubwa kwenye bendi hiyo mpya ambayo inaundwa na sehemu kubwa ya wanamuziki vijana na hivyo kuifanya izidi kupiga hatua.
Rais huyo alisema kuwa mzee Mapili amejiunga na bendi hiyo ikiwa ni wiki chache tangu imchukue Kibugila aliyeziba nafasi ya Seleman Shaibu Mumba aliyechukuliwa na bendi ya Twanga Pepeta.
"Pia mzee mapili amejiunga na kukuta tumeshakamilisha nyimbo za albamu ya kwanza ambazo ni Mapenzi Yanaua, Nilinde Nikulinde, Anasa, Shida ya Mapenzi, Usia, Acha Pupa, Mkosi Gani na Mazi.
Kuhusu mikakati zaidi ya bendi hiyo, Chai Jaba inajiandaa kumalizia kazi ya kurekodi nyimbo zote na kisha itafuata kazi ya kushuti video ya nyimbo hizo kabla ya kuanza utaratibu wa uzinduzi wa albamu.
Mbali na mikakati hiyo, alisema bendi hiyo inajiandaa kuleta wanenguaji wapya wanne kutoka Congo (DR) watakaokuja kuungana na wenzao waliopo ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji wa jukwaa.

No comments:

Post a Comment