Tuesday, July 19, 2011

Mshindi wa Kimwana wa Twanga 2011 aziba nafasi ya Aisha Madinda aliyejiunga na bendi ya Extra Bongo.

Bendi ya African Stars 'wanga Pepeta' imemchukua Mshindi wa shindano la 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011, Mary Khamis kuwa mnenguaji wa bendi hiyo.
Kwa mujibu wa Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya ASET inayomiliki bendi hiyo, kimwana huyo amechukuliwa ili kuziba nafasi ya Aisha Madinda aliyejiunga na Extra Bongo.
"Mpaka kufikia hatua ya kumchukua Mary ni baada ya kuvutiwa na kiwango chake cha uchezaji kwa kuwa alionyesha kipaji cha hali ya juu katika shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 na hatimaye kuibuka mshindi," alisema.
Asha alisema ana imani hapo baadaye kimwana huyo atakuwa mmoja wa wanenguaji mahiri hasa kwa kuzingatia kwamba ametingwa kwenye shindano la 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011' na kuwashinda wenzake tisa.
Alifafanua kuwa kwa sasa Twanga Pepeta ina wanenguaji wa kike tisa na wa kiume wanne aliowataja kwa majina ya  Abdillahi Zungu, Kassim Mohammed 'Super K', Bakari Kisongo 'Mandela' na Said Mtyanga.
Kwa upande wa wanenguaji wa kike aliwataja Fasha Sunday, Beatrice Mwangosi 'Baby Tall', Asha Said, Regina Filbert, Grace Kaswaka, Vicky Pandapanda, Lillian Tungaraza 'Internet', Sabrina Mathew na Maria Soloma.
Wakati huo huo, Asha alisema kuwa bendi yake kwa kushirikiana na Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' zitafanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za kusaidia matibabu ya mwanamuziki mkongwe, Muhidin Ngurumo.
Alisema onyesho hilo litafanyika kesho Jumamosi katika ukumbi wa Mango Garden Kinondoni ambapo pia atatambulishwa rasmi 'Kimwana wa Twanga Pepeta 2011' kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
"Twanga imeandaa onyesho hilo kwa kuguswa na afya ya Ngurumo ambaye mchango wake ni mkubwa kwenye  mwanamuziki wa dansi kwa miaka mingi na ni mshauri wa karibu wa bendi ya Twanga ," alisema Asha.
Mkurugenzi huyo alisema, kila mdau wa muziki hasa wa dansi anayefuatilia maendeleo ya muziki nchini atakumbuka jinsi mkongwe Ngurumo alivyowahi kulazwa mara mbili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na maradhi.

No comments:

Post a Comment