Wednesday, July 6, 2011

Nani kuwa mshindi wa Kimwana wa Twanga Pepeta 2011?

BAADA ya zaidi ya miaka mitatu, shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta limerudi tena ambapo sasa vimwana 10 waliofanikiwa kuingia kqwenye fainali ya kinyang'anyiro hicho watapanda jukwaani.
Mpambano huo utafanyika Ijumaa Julai 8 katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam ambapo vimwana 10 wapatanda jukwaani kila mmoja akitahidi kila linalowezekana ili ashinde.
Kwa mara ya kwanza shindano kama hilo lilifnyika mwaka 2006 ambapo mshindi alikuwa ni Lulu Semagongo ambaye ni maarufu kama 'Aunt Lulu' na kujishindia gari dogo.
Mwaka uliofuata wa 2007 lilifanyika shindano la pili ambalo mshindi wake alikuwa ni Halima Haroun ambaye naye alijinyakulia gari dogo na tangu mwaka huo halijafanyika tena shindano lingine hadi mwaka huu wa 2011.
Shindano la mwaka huu lina mabadiliko katika zawadi ambapo mshindi atazawadiwa duka la vipodozi lenye thamani ya shilingi milioni tano ambalo limelipiwa kodi ya mwaka mzima.
Waandaaji wa shindano hilo wamesema kuwa wamefanya mabadiliko hayo katika zawadi kwa kuzingatia umuhimu wa kumwendeleza mshindi ili aweze kujiajiri mwenyewe kwa biashara ya duka.
"Zawadi ya duka inaweza kumfanya kimwana akaliendesha vizuri, mwishowe likamletea mafanikio katika maisha, cha msingi ni kuzingatia mbinu za uendeshaji wa biashara," alisema mratibu wa shindano hilo.
Mratibu huyo Maimatha Jesse alisema kuwa vimwana wote katika kambi ya mazoezi walipata pia elimu ya biashara na ujasiriamali, hivyo ana uhakika mshindi wa shindano hilo ataweza kumudu kulitunza duka hilo atakalojishindia.
Mshindi wa pili anatarajia kupata kitita cha shilingi 500,000 wakati mshindi wa tatu atapata 300,000 ambapo washiriki wengine watapewa 100,000 kila mmoja kama kifuta jasho.

No comments:

Post a Comment