Wednesday, July 6, 2011

Papa-zi yaja kuokoa vipaji vya wasanii wa filamu nchini

Papa-zi yaja kuokoa vipaji vya wasanii wa filamu nchini

BAADA ya kimya cha muda mrefu, hatimaye wadau wa sanaa wameanza kuchukua hatua za kusaidia kuibua na kukuza vipaji vya wasanii wachanga katika uigizaji ili kusaidia jitihada wanachofanya katika kujiendeleza kisanii.
Baadhi ya wadau hao ni kampuni ya Papa-zi ambayo imengaza mkakati kabambe wa kusaidia wasanii chipukizi jinsi ya kufuatilia hisia zao kisanii na kurekodi kazi zao na mwisho wa siku kusambaza ili kuwahakikishia soko.
Tayari kampuni hiyo imejipanga na kuweka wazi mikakati yake inayolenga kusimamia kazi zote za wasanii wachanga na hata wenye majina ili kila mmoja anufaike kupitia jasho lake.
Ili kuhakikisha kwamba kampuni hii inatimiza malengo yake, tayari imeshafanya kongamano kubwa kwa kushirikisha wadau wa filamu na kuelezea bayana kile ambacho inapanga kufanya katika fani ya filamu.
Katika kongamano hilo pia lilihamasisha wasanii waliokata tamaa ili warejee kwenye ulingo wa sanaa ili wapige kazi ya filamu kwa ajili ya kuelimisha, kuburudisha na kufundisha jamii kwa njia hiyo ya sanaa.
Kongamano hilo pia liliibuka na mawazo mapya ya kubadilisha taswira ya filamu nchini baada ya kuzoeleka kwa majina ya wasanii wakubwa huku wale wanaochipukia wakiendelea kusota bila kutambulika.
Meneja masoko wa kampuni hiyo, Issa Kipemba alisema Papa-zi imekuja kwa sura nyingine inayolenga kuwasaidia zaidi wasanii tangu wachanga na wale wenye majina makubwa.
“Kila kukicha katika filamu hakuna jipya, utaona wasanii ni wale wale tuliozoea kuwaona au kuona kazi zao, hali inayosababisha mawazo yao kuwa ni yaleyale, maeneo ya kuigiza ni yaleyale, na zaidi ya hapo utaona wazi kwamba tunaiga zaidi,” anasema Kipemba.
Mbali na hilo anasema kampuni yake inakuja na mabadiliko ikiamini kwamba kuna wasanii zaidi ya yeye (Kipemba) na pia wapo wasambazaji wa kazi zaidi ya watu wenye asili ya Kiasia wanaofanyakazi kazi hiyo kwa kiwango kikubwa sasa.
Anasema kuwepo kwa wasambazaji wachache kumechangia wasanii wa vijijini, wilayani na hata mikoani wenye vipaji tofauti kukosa soko kwa vile imezoeleka kwamba inapotoka filamu mpya, msambazaji anahoji juu ya msanii aliyeshiriki.
***
Kama filamu ikikosa msanii mwenye jina utakuta inanunuliwa kwa bei ndogo hali ambayo inachangia kuua vipaji vya wasanii ambavyo sasa kampuni ya Papa-zi imebaini hilo na imeamua kujitosa kuviokoa kwa kusambaza kazi zao.
“Kwa mfano inatokea mtu unatumia zaidi ya Sh. Milioni 5 kuandaa filamu, halafu msambazaji anahoji kama msanii fulani yumo au hayumo, na kama hayumo basi anasema atanunua kwa chini ya Sh. Milioni 2 au 3. Utabaini hizo ni dharau, ukiritimba ambao kampuni ya Papa-zi imepania kuufuta kabisa,” anasema.
Ili kufanikiasha malengo Papa-zi itafanya utafiti zaidi ili filamu zitakazochezwa na wasanii watakaowaibua na hata wenye majina, zisambazwe kwa ubora wa kazi na sio umaarufu wa jina ambao wengi kuiga filamu kutoka India au Nigeria.
Papa-zi inasema, hata wasanii wenye majina wameanza kudharauliwa na wasambazaji na wanyonyaji wengine wa kazi za wasanii na kwamba zipo filamu hazijamaliza mwezi tangu zitoke, lakini video zake zinauzwa kwa Sh 1,000 barabarani.
Kutokana na hali hiyo, kampuni ya Papa-zi imeazimia kufanya kila njia ili kuhakikisha kwamba wasanii waliokata tamaa wanaendelea na kazi hiyo bila kuzibiwa riziki na wale wanaojiona kama bila wao filamu Tanzania haiwezekani.

No comments:

Post a Comment