Thursday, August 25, 2011

Anthony Mutaka kijana mwenye ndoto za kuleta maendeleo kwenye jimbo la Musoma Vijijini

Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara ambalo kwa muda mrefu limekuwa chini ya mbunge Nimrod Mkono ambaye katika kura za maoni za mwaka jana ndani ya CCM alikumbana na upinzani toka wagombea wengine toka CCM waliojitokeza kuchuana naye.
Mmoja wa wanachama hao ni kijana Anthony Mutaka aliyewahi kuwa kiongozi msaidizi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2006, hata hivyo kura zake hazikutosha.
Mutaka ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Suguti Wilaya ya Musoma Vijijini, pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM taifa akiwakilisha wilaya hiyo ya Musoma Vijijini.
Mbali na nafasi hiyo Mutaka pia ni Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Vijijini na mkoa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM akiwakilisha mkoa wa Mara.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vijana wengi wakiwemo wa CCM na vyama vya upinzani walijitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali kuanzia udiwani hadi ubunge.
Hata hivyo, kwa Mutaka ingawa alijaribu kuwania ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini, kura zake hazikutosha, hivyo inabidi asubiri hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 panapo majaliwa.
Kama bado atakuwa na nia ya kuwania tena ubunge, basi atachukua famu ili kujaribu kwa mara ya pili
kutokana na ukweli kwamba alikuwa akikubalika kwa makundi yote wakiwemo vijana.
Anasema kuwa yeye kama Mtanzania ana haki ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi lakini kwa sasa hawezi kusema lolote kwa vile siyo wakati muafaka kuzungumzia hilo.
"Ni kweli wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini walitamani niwe mbunge wao, lakini bahati mbaya kura zangu hazikutosha na hivyo mbunge aliyepo sasa ni mheshimiwa Mkono," anasema Mutaka.
Kijana huyu ni msomi mwenye Shahada ya Kwanza ya Uongozi na Utawala, Menejimenti ya Umma alioipata kutoka Mzumbe mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment