Wednesday, August 24, 2011

Hatimaye Mashujaa Musica yafanikiwa kuimarisha bonanza

Bendi ya Mashujaa Musica ambayo imebaki na siku moja ya onyesho kwa wiki kipindi chote cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, imesema kuwa imefanikiwa kuimarisha bonanza jipya la kila Jumapili.
Kwa mujibu wa Makamu wa rais wa bendi hiyo, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', bonanza hilo linafanyika katika ukumbi wa  Green Acres House, Busness Park eneo la Victoria, jijini Dar es Salaam.
"Lengo letu lilikuwa ni kuimarisha zaidi bonanza letu na kwa kweli limekubalika vilivyo, kwa hiyo tuna uhakika kwamba eneo la Victoria na vitongoji vyake pamoja na maeneo mengine ni mali ya Mashujaa Musica," alisema.
Alisema kuwa wingi wa mashabiki wanaojitokeza kwenye bonanza hilo imewapa moyo wa kuendelea kufanya vitu vyao eneo hilo hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
"Tumeshateka mashabiki wa kutosha hasa baada ya kupunguza siku za maonyesho na kubaki na bonanza la kila Jumapili ambalo sasa limetuonyesha njia kwamba bendi yetu inakubalika," alisema 'Sauti ya Radi'.
Kabla ya kuhamia Victoria, kwa muda mrefu bendi hiyo ilikuwa ikifanya bonanza lhilo katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Magereza Ukonga na sasa imeamua kubadili upepo.
Mashujaa Musica imekuwa ikitamba na albamu yake ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na sasa imeanza kuandaa ya  pili ikiwa imekamilisha karibu nyimbo zote za albamu hiyo.
Mbali na hayo, bendi hiyo pia imekuwa ikimarisha idara zake kwa kuongeza wanamuziki wapya ambapo hivi karibuni iliwanasa wapiga vyombo watatu Kassim Mumba na Khalfan Kamodee (besi) na mpiga drums Totoo.
Katika kuimarisha idara zake bendi hiyo pia iliongeza mnenguaji Salma Mwiba na hivyo kuifanya iwe na jumla ya wanenguaji sita wa kike ambao ni Pendo Bonzo, Sweet Baby, Salma Teketeke, Flora Bambucha na Rose Twiga

No comments:

Post a Comment