Zawadi za Vimwana wa Twanga hadharani
VIMWANA waliofanikiwa kuingia 10Bora wanatarajiwa kuchuana vikali, Julai 8 katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Sambamba na hilo, zawadi za vimwana hao zimewekwa hadharani na mkurugenzi wa kampuni ya ASET, Asha Baraka ambaye kampuni yake hiyo inamiliki bendi ya Twanga Pepeta.
Akitangaza zawadi hizo mbele ya waandishi wa habari, Asha alisema kuwa mshindi wa kwanza atajinyakulia duka la vipodizi lenye thamani ya shilingi milioni tano likiwa limelipiwa kodi ya mwaka.
"Mshindi wa pili atapata 500,000 wakat mshindi wa tatu atajinyakulia kitita cha shilingi 300,000 na washiriki wengine kila mmoja atapata shilingi 100,000 ya kifiuta jasho," alisema Asha.
Naye mratibu wa shindano la KImwana wa Twanga Pepeta, Maimatha Jesse aliwataja vimwana hao kuwa ni Edina Amani, Mariam Joseph, Salha George, Amanda Cyprian, Rehema Said, Mary Hamis, Amina Juma, Johari Juma, Hawa Miraji na Leila Mshana.
Maimatha alisema kuwa maandalizi yote ya kufanikisha shindano hilo yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaandaa vimwana ili waweze kujiamini watakapopanda jukwaani kuchuana.
No comments:
Post a Comment