Wednesday, August 24, 2011

Kalunde kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili baada ya makamuzi kwenye sikukuu ya Idd

Baada ya kukamilisha kazi ya kurekodi nyimbo za albamu ya pili, uongozi wa bendi ya Kalunde umesema kuwa sasa wanamuziki wanajiandaa kwa ajili ya kushuti video ya nyimbo hizo.
Kwa zaidi ya miezi miwili bendi hiyo ilikuwa kwenye  mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili maandalizi ambayo yalienda sambamba na maonyesho ya kila mwisho wa wiki.
Kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo ambayo haijapewa jina kuwa ni 'Sisee', 'Masumbuko', 'Fungua', 'Ulinipendea Nini, 'Ndoto' na 'Miaka 50 ya Uhuru'.
"Kwa kuwa tumekamilisha kurekodi nyimbo za albamu nzima, sasa tunajipanga kwa hatua nyingine ambayo ni ya kushuti video ya nyimbo zote hizo ambazo zimeandaliwa kwa zaidi ya miezi miwili," alisema Rudala.
Licha ya kuwa na maonyesho kila mwisho wa wiki, alisema kuwa anashukuru wamefanikiwa kukamilisha albamu hiyo ambayo amedai kuwa nyimbo zake ni kali na kwamba zimetokea kupendwa hata kabla albamu haijatoka.
Aliongeza kuwa ingawa kipindi chote cha Ramadhan bendi hiyo imeendelea na maonyesho kama kawaida kutokana na kubanwa na mkataba, bado imeweza kufanikiwa kukamilisha kurekodi nyimbo za albamu hiyo.
"Hii ni hatua nzuri kwetu hasa kwa kuzingatia kwamba wanamuziki wa bendi ya Kalunde wamekuwa wakijituma vilivyo kufanya kazi hadi kufikia hatua tulipo sasa," alisema.
Aidha alisema kuwa wakati wa sikukuu ya Idd bendi hiyo inatarajia kufanya makamuzi ya nguvu katika ukumbi wa Triniti uliopo Oysterbay na kisha Idd pili itakuwa New Kunduchi Beach Hotel.
Kalunde ni bendi inayoundwa na wanamuziki wenye vipaji wakiwemo, Deo Mwanambilimbi, Mwakichui Saleh, Anania Ngoriga, Othman Majuto, Deborah Nyangi, Mwapwani Yahaya, Junior Gringo na wengine wengi.

No comments:

Post a Comment