Thursday, August 25, 2011

Elimu ni ufunguo wa maisha na kwa msemo huu ndio maana wazazi na walezi wanaojua umuhimu wa elimu wamekuwa wakiwapeleka watoto wao shule ili wapate elimu. Pichani Mtoto Edda Kasika akiwa na mfuko wake wa madaftari akisubiri gari ili kwenda shuleni.


Mjumbe wa Baraka Kuu la Umoja kutoka mkoa wa Mara ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa toka Wilaya Musoma Vijijini, Anthony Mutaka kwenye moja ya mikutano ya Jumuiya. Yeye alikuwa miongoni mwa wana CCM waliojitokeza kumvaa mbunge Nimrod Mkono kwenye jimbo la Musoma Vijijini mwaka 2010.


Anthony Mutaka kijana mwenye ndoto za kuleta maendeleo kwenye jimbo la Musoma Vijijini

Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara ambalo kwa muda mrefu limekuwa chini ya mbunge Nimrod Mkono ambaye katika kura za maoni za mwaka jana ndani ya CCM alikumbana na upinzani toka wagombea wengine toka CCM waliojitokeza kuchuana naye.
Mmoja wa wanachama hao ni kijana Anthony Mutaka aliyewahi kuwa kiongozi msaidizi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2006, hata hivyo kura zake hazikutosha.
Mutaka ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Suguti Wilaya ya Musoma Vijijini, pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM taifa akiwakilisha wilaya hiyo ya Musoma Vijijini.
Mbali na nafasi hiyo Mutaka pia ni Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Vijijini na mkoa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM akiwakilisha mkoa wa Mara.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vijana wengi wakiwemo wa CCM na vyama vya upinzani walijitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali kuanzia udiwani hadi ubunge.
Hata hivyo, kwa Mutaka ingawa alijaribu kuwania ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini, kura zake hazikutosha, hivyo inabidi asubiri hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 panapo majaliwa.
Kama bado atakuwa na nia ya kuwania tena ubunge, basi atachukua famu ili kujaribu kwa mara ya pili
kutokana na ukweli kwamba alikuwa akikubalika kwa makundi yote wakiwemo vijana.
Anasema kuwa yeye kama Mtanzania ana haki ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi lakini kwa sasa hawezi kusema lolote kwa vile siyo wakati muafaka kuzungumzia hilo.
"Ni kweli wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini walitamani niwe mbunge wao, lakini bahati mbaya kura zangu hazikutosha na hivyo mbunge aliyepo sasa ni mheshimiwa Mkono," anasema Mutaka.
Kijana huyu ni msomi mwenye Shahada ya Kwanza ya Uongozi na Utawala, Menejimenti ya Umma alioipata kutoka Mzumbe mkoani Morogoro.

Wednesday, August 24, 2011

Baadhi ya waimbaji wa bendi ya Mashujaa Musica wakiwajibika jukwaani.


Hatimaye Mashujaa Musica yafanikiwa kuimarisha bonanza

Bendi ya Mashujaa Musica ambayo imebaki na siku moja ya onyesho kwa wiki kipindi chote cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, imesema kuwa imefanikiwa kuimarisha bonanza jipya la kila Jumapili.
Kwa mujibu wa Makamu wa rais wa bendi hiyo, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', bonanza hilo linafanyika katika ukumbi wa  Green Acres House, Busness Park eneo la Victoria, jijini Dar es Salaam.
"Lengo letu lilikuwa ni kuimarisha zaidi bonanza letu na kwa kweli limekubalika vilivyo, kwa hiyo tuna uhakika kwamba eneo la Victoria na vitongoji vyake pamoja na maeneo mengine ni mali ya Mashujaa Musica," alisema.
Alisema kuwa wingi wa mashabiki wanaojitokeza kwenye bonanza hilo imewapa moyo wa kuendelea kufanya vitu vyao eneo hilo hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
"Tumeshateka mashabiki wa kutosha hasa baada ya kupunguza siku za maonyesho na kubaki na bonanza la kila Jumapili ambalo sasa limetuonyesha njia kwamba bendi yetu inakubalika," alisema 'Sauti ya Radi'.
Kabla ya kuhamia Victoria, kwa muda mrefu bendi hiyo ilikuwa ikifanya bonanza lhilo katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Magereza Ukonga na sasa imeamua kubadili upepo.
Mashujaa Musica imekuwa ikitamba na albamu yake ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na sasa imeanza kuandaa ya  pili ikiwa imekamilisha karibu nyimbo zote za albamu hiyo.
Mbali na hayo, bendi hiyo pia imekuwa ikimarisha idara zake kwa kuongeza wanamuziki wapya ambapo hivi karibuni iliwanasa wapiga vyombo watatu Kassim Mumba na Khalfan Kamodee (besi) na mpiga drums Totoo.
Katika kuimarisha idara zake bendi hiyo pia iliongeza mnenguaji Salma Mwiba na hivyo kuifanya iwe na jumla ya wanenguaji sita wa kike ambao ni Pendo Bonzo, Sweet Baby, Salma Teketeke, Flora Bambucha na Rose Twiga

Baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Kalunde wakiwa kazini kwenye onyesho lao katika ukumbi wa Triniti uliopo Oysterbay.


Kalunde kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili baada ya makamuzi kwenye sikukuu ya Idd

Baada ya kukamilisha kazi ya kurekodi nyimbo za albamu ya pili, uongozi wa bendi ya Kalunde umesema kuwa sasa wanamuziki wanajiandaa kwa ajili ya kushuti video ya nyimbo hizo.
Kwa zaidi ya miezi miwili bendi hiyo ilikuwa kwenye  mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili maandalizi ambayo yalienda sambamba na maonyesho ya kila mwisho wa wiki.
Kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo ambayo haijapewa jina kuwa ni 'Sisee', 'Masumbuko', 'Fungua', 'Ulinipendea Nini, 'Ndoto' na 'Miaka 50 ya Uhuru'.
"Kwa kuwa tumekamilisha kurekodi nyimbo za albamu nzima, sasa tunajipanga kwa hatua nyingine ambayo ni ya kushuti video ya nyimbo zote hizo ambazo zimeandaliwa kwa zaidi ya miezi miwili," alisema Rudala.
Licha ya kuwa na maonyesho kila mwisho wa wiki, alisema kuwa anashukuru wamefanikiwa kukamilisha albamu hiyo ambayo amedai kuwa nyimbo zake ni kali na kwamba zimetokea kupendwa hata kabla albamu haijatoka.
Aliongeza kuwa ingawa kipindi chote cha Ramadhan bendi hiyo imeendelea na maonyesho kama kawaida kutokana na kubanwa na mkataba, bado imeweza kufanikiwa kukamilisha kurekodi nyimbo za albamu hiyo.
"Hii ni hatua nzuri kwetu hasa kwa kuzingatia kwamba wanamuziki wa bendi ya Kalunde wamekuwa wakijituma vilivyo kufanya kazi hadi kufikia hatua tulipo sasa," alisema.
Aidha alisema kuwa wakati wa sikukuu ya Idd bendi hiyo inatarajia kufanya makamuzi ya nguvu katika ukumbi wa Triniti uliopo Oysterbay na kisha Idd pili itakuwa New Kunduchi Beach Hotel.
Kalunde ni bendi inayoundwa na wanamuziki wenye vipaji wakiwemo, Deo Mwanambilimbi, Mwakichui Saleh, Anania Ngoriga, Othman Majuto, Deborah Nyangi, Mwapwani Yahaya, Junior Gringo na wengine wengi.

Tuesday, August 23, 2011

Vimwana wa bendi ya Extra Bongo ambao leo usiku watafanya vitu vyao kwenye onyesho la Listening Part wakiwa katika pozi.


Listening part ya Extra Bongo leo Agosti 24 katika ukumbi wa Meeda Club Sinza-Mori

Bendi ya Extra Bongo leo itafanya onyesho maalum la kusikilizisha nyimbo zake za albamu ya pili 'Listening Part' mbele ya waandishi wa habari na wadau mbalimbali za muziki wa dansi.
Kiongozi wa bendi hiyo Rogert Hegga ameiambia Sugutiraha.blogspot kuwa onyesho hilo litafanyika leo Jumatano, Agosti 24 katika ukumbi wa Meeda Club Sinza- Mori, jijini Dar es Salaam.
Hegga alisema kuwa onyesho hilo linafanyika ikiwa ni siku chache baada ya bendi hiyo kumaliza kushuti video ya wimbo wa Watu na Falsafa uliotungwa na mwimbaji Banza Stone.
"Tulianza kwa video ya wimbo wa Mtenda Akitendewa ukafuatia huu wa Watu na Falsafa na sasa tunataka kuwaonyesha wadau wa muziki kile ambacho tumekifanya kwa kipindi chote cha Ramadhan," alisema.
Kiongozi huyo alifafanua kuwa nyimbo nyingine zilizobaki za 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Mashuu' na 'Bakutuka' zitainaingizwa kwenye video baada ya kumalizika sikukuu ya Idd.
Hegga alisema ana uhakika kuwa hatua ambayo bendi hiyo imefikia ya kujiimarisha ni kubwa kwa madai kwamba wapenzi wa muziki wa dansi wanazidi kuikubali kutokana na ubora wa muziki inaopiga.
Kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan, Extra Bongo inafanya onyesho moja kwa wiki ambalo hufanyika kila Jumamosi katika ukumbi wake wa nyumbani wa Meeda Club Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Aidha, Extra Bongo inajiandaa kutoa burudani siku ya Idd mosi katika ukumbi Meeda na kisha Idd pili itaibukia ndani ya ukumbi wa Wenge Garden uliopo Ukonga ili kuendelea kuwaburudisha wapenzi wa muziki wa dansi.
Bendi hiyo 'ilifufuka' upya ikiwa na albamu ya 'Mjini Mipango' ambayo nyimbo zake ni 'Laptop', 'First Lady', 'Maisha Taiti', 'Safari ya Maisha' na 'Wema' zilizochangia kuiweka kwenye chati.

Tuesday, August 16, 2011

Baadhi ya waimbaji wa bendi ya Mashujaa Musica wakiimba kwenye bonanza la bendi hiyo katika ukumbi wa Green Acres House uliopo eneo la Victoria, jijini Dar es Salaam.


Mashujaa Musica yatumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kujiimarisha

Bendi ya Mashujaa Musica ambayo imebaki na siku moja ya onyesho kwa wiki wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, imesema kuwa inatumia nafasi hiyo kuimarisha bonanza jipya la kila Jumapili.
Kwa mujibu wa Makamu wa rais wa bendi hiyo, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', bonanza hilo linafanyika katika ukumbi wa  Green Acres House, Busness Park eneo la Victoria, jijini Dar es Salaam.
"Lengo letu ni kujiimarisha zaidi baada ya kubaini kwamba bendi yetu imeanza kukubalika vilivyo kwenye eneo la Victoria na vitongoji vyake pamoja na maeneo mengine kwa ujumla," alisema.
Alisema kuwa wingi wa mashabiki wanaojitokeza kwenye bonanza hilo imewapa moyo wa kuendelea kukazania bonanza hilo ili lizidi kukubalika na hasa wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
"Tunataka itakapofika wakati wa sikukuu ya Idd tuwe tumeshateka mashabiki wengi zaidi, ndio maana tumesimamisha maonyesho mengine na kubakiza bonanza la kila Jumapili ili liwe imara," alisema 'Sauti ya Radi'.
Kabla ya kuhamia Victoria, kwa muda mrefu bendi hiyo ilikuwa ikifanya bonanza lhilo katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Magereza Ukonga na sasa imeamua kubadili upepo.
Mashujaa Musica imekuwa ikitamba na albamu yake ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na sasa imeanza kuandaa ya  pili ikiwa imekamilisha karibu nyimbo zote za albamu hiyo.
Mbali na hayo, bendi hiyo pia imekuwa ikimarisha idara zake kwa kuongeza wanamuziki wapya ambapo hivi karibuni iliwanasa wapiga vyombo watatu Kassim Mumba na Khalfan Kamodee (besi) na mpiga drums Totoo.
Katika kuimarisha idara zake bendi hiyo pia iliongeza mnenguaji Salma Mwiba na hivyo kuifanya iwe na jumla ya wanenguaji sita wa kike ambao ni Pendo Bonzo, Sweet Baby, Salma Teketeke, Flora Bambucha na Rose Twiga.

Super Nyamwela akifanya vitu vyake kwenye onyesho la bendi ya Extra Bongo ambapo sasa ameibuka na kibao cha 'Bakutuka'.


Nyamwela akamilisha albamu ya Extra Bongo kwa wimbo wa 'Bakutuka'

Bendi ya Extra Bongo ambayo kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan inaendelea mazoezi ya nyimbo za albamu ya pili, imekamilisha kibao cha 'Bakutuka' kilichotungwa na kiongozi wa shoo wa bendi hiyo, Super Nyamwela.
Akizungumza na Sugutiraha.blogspot, Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki alisema kuwa kibao hicho kimekamilisha albamu ya pili ambayo itakuwa na nyimbo sita.
"Tulianza na wimbo wa Mtenda Akitendewa ukafuatia wa Fisadi wa Mapenzi, Watu na Falsafa, Neema, Mashuu na sasa tuna huu wa Bakutuka ambao umetungwa na kiongozi wetu wa shoo," alisema Choki.
Choki alisema, wimbo huo unaimbwa kwa lugha ya kiswahili na kuchanganywa kidogo na kimwera ambapo amefafanua kuwa 'Bakutuka' kwa lugha hiyo ya kimwera maana yake ni wanakimbia.
Hata hivyo hakuelezea zaidi wanaokimbia ni nani, lakini akaongeza kuwa ili kujua ujumbe uliomo katika kibao hicho ni kuusikiliza pale unapoimbwa na siyo kusimuliwa tu.
Mkurugenzi huyo alisema  kibao hicho kitasikika kwa mara ya kwanza kesho Jumamosi kwenye onyesho la bendi hiyo katika ukumbi wa Meeda Club Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema juzi wanamuziki wake walikuwa na kazi ya kushuti video ya kibao cha 'Watu na Falsafa' kilichotungwa  na Banza Stone  huku wakitarajia kuendelea na vibao vingine wiki ijayo.
Alifafanua kuwa kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan bendi hiyo imekuwa ikifanya onyesho moja huku ikitumia muda mwingi kukamilisha albamu ya pili ambapo imesharekodi vibao vitano na kubakiza kimoja cha 'Bakutuka'.

Asha Baraka ambaye kampuni yake ya ASET imeunga mkono juhudi za Alex Msama (kushoto) za kukamata wezi wa kazi za wasanii.


Kampuni ya ASET yaunga mkono juhudi za Msama Auction Mart ya kukamata wezi wa kazi za wasanii

Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) inayomilika bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' imesema iko tayari kuunga mkono juhudi za kampuni ya Msama Auction Mart kwa juhudi zake za kusaka wezi wa kazi za wasanii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka alipokuwa akizungumza na SUGUTIRAHA.blogspot kuhusu juhudi za Msama Auction Mart za kukamata watu wanaowaibia wasanii.
"Sisi kama ASET tunaunga mkono juhudi za mkurufenzi wa Msama Auction Mart, Alex Msama na tuko tayari kumpa ushirikiano wa hali na mali ili aendelee kuwanasa wezi wa kazi za wasanii ambalo anaendelea nalo," alisema Asha.
Asha alisema kuwa kampuni yake imefungua milango wazi kwa Msama ili kumsaidia kifedha ama kumpa vijana wa kuzunguka nao kwenye msako wa kuwanasa wezi hao.
"Pia nina mpango wa kuwasiliana na baadhi ya wamiliki wa bendi ili tukutane na kuweka mkakati wa kuungana na Msama, kwani sisi wote ni waathirika wa hii hali, tunaibiwa kazi zetu na wajanja wachache," alisema.
Aliongeza kuwa bendi yake kwa sasa inaandaa albamu ya 11 hivyo hayuko tayari kuimba anaibiwa ambapo amewataka wadau wote wa muziki kuunga mkono juhudi za Msama kwa hali na mali ili kukomesha wizi huo.
Katika zoezi lake la kukamata wezi wa jkazi za wasanii, wiki iliyopita kampuni ya Msama Auction Mart ilikamata mitambo miwili ya kudurufu VCD za wasanii wa muziki wa Injili na wa dansi maeneo ya Mabibo na Kinondoni.
Katika hilo, walinasa pia  VCD 164 tupu na nyingine 54 zilizokuwa zimesharekodiwa zikiandaliwa kupelekwa mitaani kwa ajili ya kuuzwa ambapo watuhumiwa walifikishwa kwenye vituo vya polisi vya  Urafiki na Oysterbay.
Mendelezo wa zoezi la kunasa wezi wa kazi za wasanii, Msama Auction Mart ilishakamata VCD 1,108 zenye thamani ya Sh. milioni 20 na tayari watuhumiwa walishafikishwa mahakamani ili  kujibu mashtaka yanayowakabili.

Monday, August 15, 2011

Afisa Mtendaji wa kata ya Manzese, Hussein Omary (kushoto) akizungumza na wenyeviti wa serikali za mitaa na baadhi ya sungusungu waliopewa jukumu la kukamata watu watakaochafua mazingira ya kata hiyo


Afisa Mtendaji wa kata ya Manzese asema Manzese bila uchafu inawezekana

Manzese bila uchafu inawezekana, hivi ndivyo anavyoamini, Afisa Mtendaji wa kata ya Manzese, jijini Dar es salaam, Bw. Hussein Omary ambapo sasa imebuni utaratibu wa kuhakikisha kata hiyo inang'aa kwa usafi.
Utaratibu huo ni kuunda jeshi la jadi la sungusungu ambalo litakuwa na jukumu la kuwakamata wachafuzi wote wa mazingira na kuwafikishwa ofisini kwake ili wachukuliwe hatua zaidi za kisheria.
Tayari mtendaji huyo ana sungusungu hao 52 ambao walianza kazi tangu Agosti 10 mwaka huu na wamekuwa  wakizunguka kwenye maeneo mbalimbali ya kata hiyo ili kuhakikisha kwamba hakuna anayetupa taka ovyo.
Omary alisema mtuhumiwa atakayekamatwa akitupa taka ovyo, kutiririsha maji ama kujisaidia ovyo atatozwa faini ya shilingi 50,000, wale watakaomkamata watapewa asilimia 30 toka kwenye faini hiyo.
Mtendaji huyo alisema kuwa ana uhakika kwa ushirikiano kati yake na wenyeviti wa serikali za mitaa watafanikiwa kuiweka kata Manzese katika hali ya usafi na kuwa ya mfano kwenye jiji la Dar es Salaam.
"Wapo watu ambao wamekuwa wakibeba mifuko ya plastiki yenye taka na kujifanya kama wana mizigo ya kawaida na kumbe ni taka wanakwenda kuzitupa kwenye mitaro hao tumewagundua watakamatwa," alisema Omary.
Alifafanua kuwa watu hao wamekuwa wakitupa taka kuanzia saa tisa usiku hadi ya 12  alfajiri na kwamba sungusungu watakuwa wanazunguka kwenye mitaa hiyo ya kata hiyo ili kuwanasa wachafuzi hao wa mazingira.
Omaru aliitaja baadhi ya mitaa ya kata ya Manzese ambayo sungusungu wake wamepewa kazi ya kuizungukia kuwa ni  Kilimani, Mwembeni, Mnazi Mmoja, Midizini, Uzuri, Mvuleni na Muungano.
"Mbona miji mingine ukiwemo wa Moshi mkoani Kilimanjaro unang'aa kwa usafi na kwa nini sisi kwenye kata yetu tushindwe?  Nina uhakika kwa ushirikiano wenu tutafaulu na kuwa mfano mzuri kwa jiji la Dar es Salaam," alisema.
Alisema kuwa cha kuzingatia ni sungusungu hao kutimiza wajibu wao bila kushawishika kwa kuchukua chochote kwa watuhumiwa bali wawafikishe kwenye ofisi ya mtendaji ili sheria ichukue mkondo wake.
Mtendaji huyo ameibuka na mpango huo wa kuiweka Manzese katika hali ya usafi ikiwa ni miezi michache tangu ahamishiwe hapo akitokea kata ya Sinza.

Tuesday, August 2, 2011

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Elimu, Kassim Majaliwa (katikati) akiwa na wachapakazi.

Mtaalamu wa kutoa damu toka Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki, Judith Chale akiendesha zoezi la uchangiaji damu kwa wanafunzi wa Mbezi High School

Mbezi High School waonyesha njia kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia damu

Walimu na wanafunzi wa Mbezi High School wamekuwa mstari wa mbele katika uchangiaji wa damu kwa ajili ya kusaidia akiba ya damu ya taifa ambapo kila mara wamekuwa wakijitolea kuchangia damu.
Mkuu wa shule  hiyo Said Amran anasema kuwa ni kawaida kwa walimu na wanafunzi wake kuchangia damu kwa vile wanatambua umuhimu wa kufanya hivyo ili kuwasaidia Watanzania wenzao.
Mkuu huyo wa shule alisema hayo wakati wa zoezi la uchangiaji damu mbali liliendeshwa na Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki shuleni hapo hivi karibuni.
Zaidi ya wanafunzi 20 walichangia damu hiyo wakati wa zoezi hilo ambalo lilifanywa na wataalum wa kutoa damu akiwe mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Judith Chale.

'Hata mimi ninaweza'. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Elimu, Kassim Majaliwa akicheza ngoma za asili alipotembelea jimbo lake la Ruangwa mkoani Lindi.

Mwana dada Kidawa Abdul ambaye sasa yuko studio akiendelea kurekodi kibao chake cha 'Niamini'.

Kidawa yuko studio akirekodi kibao chake cha tatu kiitwacho 'Niamini' .

Mwimbaji wa kike wa Top Band, Kidawa Abdul, amesema kuwa licha ya kwamba ni muda mrefu umepita, bado anaendelea kuhangaikia albamu yake binafsi ya 'Usiniache' na sasa anarekodi kibao cha tatu kiitwacho 'Niamini'.
Kidawa aliliambia gazeti la NIPASHE kuwa kazi ya kurekodi albamu yake hiyo ilianza Januari mwaka huu kwa vibao vya 'Usiniache' na 'Sitaki Tena' ambapo sasa anaendelea na hicho cha tatu.
"Kazi ya kurekodi albamu hii imechukua muda mrefu kutokana na hali halisi ya kiuchumi, lakini kila nitakapopata fedha nitaingia studio kurekodi kwani nina nyimbo za kutosha albamu nzima," alisema.
Mwimbaji huyo alivitaja baadhi ya vibao vyake hivyo kuwa ni 'Nakupenda', 'Naringa', 'Nimemaliza' na 'Tanzania' ambapo aliongeza kusema kuwa vingine ambavyo amemshirikisha kaka yake Thabit Abdul.
Kidawa ambaye amewahi kuimbia bendi ya Mchinga Sound ambayo kwa sasa haipo, alisema kuwa kibao chake cha 'Usiniache' atakisambaza kwenye vituo mbalimbali vya redio mara baada ya kushuti video.
"Karibu nyimbo nyingi nimeimba katika mtindo wa zouk isipokuwa mmoja tu wa Naringa ambao ni wa mduara, nina uhakika albamu yangu itafanya vizuri sokoni itakapokamilika," alijigamba.
Mwana dada huyo alisema anawashukuru wanamuziki wa Top Band  kwa ushirikiano anaoupata ukiwemo wa kumtia moyo ili kuhakikisha kwamba anakamilisha albami yake ili baadaye itinge sokoni.