Monday, August 15, 2011

Afisa Mtendaji wa kata ya Manzese asema Manzese bila uchafu inawezekana

Manzese bila uchafu inawezekana, hivi ndivyo anavyoamini, Afisa Mtendaji wa kata ya Manzese, jijini Dar es salaam, Bw. Hussein Omary ambapo sasa imebuni utaratibu wa kuhakikisha kata hiyo inang'aa kwa usafi.
Utaratibu huo ni kuunda jeshi la jadi la sungusungu ambalo litakuwa na jukumu la kuwakamata wachafuzi wote wa mazingira na kuwafikishwa ofisini kwake ili wachukuliwe hatua zaidi za kisheria.
Tayari mtendaji huyo ana sungusungu hao 52 ambao walianza kazi tangu Agosti 10 mwaka huu na wamekuwa  wakizunguka kwenye maeneo mbalimbali ya kata hiyo ili kuhakikisha kwamba hakuna anayetupa taka ovyo.
Omary alisema mtuhumiwa atakayekamatwa akitupa taka ovyo, kutiririsha maji ama kujisaidia ovyo atatozwa faini ya shilingi 50,000, wale watakaomkamata watapewa asilimia 30 toka kwenye faini hiyo.
Mtendaji huyo alisema kuwa ana uhakika kwa ushirikiano kati yake na wenyeviti wa serikali za mitaa watafanikiwa kuiweka kata Manzese katika hali ya usafi na kuwa ya mfano kwenye jiji la Dar es Salaam.
"Wapo watu ambao wamekuwa wakibeba mifuko ya plastiki yenye taka na kujifanya kama wana mizigo ya kawaida na kumbe ni taka wanakwenda kuzitupa kwenye mitaro hao tumewagundua watakamatwa," alisema Omary.
Alifafanua kuwa watu hao wamekuwa wakitupa taka kuanzia saa tisa usiku hadi ya 12  alfajiri na kwamba sungusungu watakuwa wanazunguka kwenye mitaa hiyo ya kata hiyo ili kuwanasa wachafuzi hao wa mazingira.
Omaru aliitaja baadhi ya mitaa ya kata ya Manzese ambayo sungusungu wake wamepewa kazi ya kuizungukia kuwa ni  Kilimani, Mwembeni, Mnazi Mmoja, Midizini, Uzuri, Mvuleni na Muungano.
"Mbona miji mingine ukiwemo wa Moshi mkoani Kilimanjaro unang'aa kwa usafi na kwa nini sisi kwenye kata yetu tushindwe?  Nina uhakika kwa ushirikiano wenu tutafaulu na kuwa mfano mzuri kwa jiji la Dar es Salaam," alisema.
Alisema kuwa cha kuzingatia ni sungusungu hao kutimiza wajibu wao bila kushawishika kwa kuchukua chochote kwa watuhumiwa bali wawafikishe kwenye ofisi ya mtendaji ili sheria ichukue mkondo wake.
Mtendaji huyo ameibuka na mpango huo wa kuiweka Manzese katika hali ya usafi ikiwa ni miezi michache tangu ahamishiwe hapo akitokea kata ya Sinza.

No comments:

Post a Comment