Mwimbaji wa kike wa Top Band, Kidawa Abdul, amesema kuwa licha ya kwamba ni muda mrefu umepita, bado anaendelea kuhangaikia albamu yake binafsi ya 'Usiniache' na sasa anarekodi kibao cha tatu kiitwacho 'Niamini'.
Kidawa aliliambia gazeti la NIPASHE kuwa kazi ya kurekodi albamu yake hiyo ilianza Januari mwaka huu kwa vibao vya 'Usiniache' na 'Sitaki Tena' ambapo sasa anaendelea na hicho cha tatu.
"Kazi ya kurekodi albamu hii imechukua muda mrefu kutokana na hali halisi ya kiuchumi, lakini kila nitakapopata fedha nitaingia studio kurekodi kwani nina nyimbo za kutosha albamu nzima," alisema.
Mwimbaji huyo alivitaja baadhi ya vibao vyake hivyo kuwa ni 'Nakupenda', 'Naringa', 'Nimemaliza' na 'Tanzania' ambapo aliongeza kusema kuwa vingine ambavyo amemshirikisha kaka yake Thabit Abdul.
Kidawa ambaye amewahi kuimbia bendi ya Mchinga Sound ambayo kwa sasa haipo, alisema kuwa kibao chake cha 'Usiniache' atakisambaza kwenye vituo mbalimbali vya redio mara baada ya kushuti video.
"Karibu nyimbo nyingi nimeimba katika mtindo wa zouk isipokuwa mmoja tu wa Naringa ambao ni wa mduara, nina uhakika albamu yangu itafanya vizuri sokoni itakapokamilika," alijigamba.
Mwana dada huyo alisema anawashukuru wanamuziki wa Top Band kwa ushirikiano anaoupata ukiwemo wa kumtia moyo ili kuhakikisha kwamba anakamilisha albami yake ili baadaye itinge sokoni.
No comments:
Post a Comment