Bendi ya Mashujaa Musica ambayo imebaki na siku moja ya onyesho kwa wiki wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, imesema kuwa inatumia nafasi hiyo kuimarisha bonanza jipya la kila Jumapili.
Kwa mujibu wa Makamu wa rais wa bendi hiyo, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', bonanza hilo linafanyika katika ukumbi wa Green Acres House, Busness Park eneo la Victoria, jijini Dar es Salaam.
"Lengo letu ni kujiimarisha zaidi baada ya kubaini kwamba bendi yetu imeanza kukubalika vilivyo kwenye eneo la Victoria na vitongoji vyake pamoja na maeneo mengine kwa ujumla," alisema.
Alisema kuwa wingi wa mashabiki wanaojitokeza kwenye bonanza hilo imewapa moyo wa kuendelea kukazania bonanza hilo ili lizidi kukubalika na hasa wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
"Tunataka itakapofika wakati wa sikukuu ya Idd tuwe tumeshateka mashabiki wengi zaidi, ndio maana tumesimamisha maonyesho mengine na kubakiza bonanza la kila Jumapili ili liwe imara," alisema 'Sauti ya Radi'.
Kabla ya kuhamia Victoria, kwa muda mrefu bendi hiyo ilikuwa ikifanya bonanza lhilo katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Magereza Ukonga na sasa imeamua kubadili upepo.
Mashujaa Musica imekuwa ikitamba na albamu yake ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na sasa imeanza kuandaa ya pili ikiwa imekamilisha karibu nyimbo zote za albamu hiyo.
Mbali na hayo, bendi hiyo pia imekuwa ikimarisha idara zake kwa kuongeza wanamuziki wapya ambapo hivi karibuni iliwanasa wapiga vyombo watatu Kassim Mumba na Khalfan Kamodee (besi) na mpiga drums Totoo.
Katika kuimarisha idara zake bendi hiyo pia iliongeza mnenguaji Salma Mwiba na hivyo kuifanya iwe na jumla ya wanenguaji sita wa kike ambao ni Pendo Bonzo, Sweet Baby, Salma Teketeke, Flora Bambucha na Rose Twiga.
No comments:
Post a Comment