Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) inayomilika bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' imesema iko tayari kuunga mkono juhudi za kampuni ya Msama Auction Mart kwa juhudi zake za kusaka wezi wa kazi za wasanii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka alipokuwa akizungumza na SUGUTIRAHA.blogspot kuhusu juhudi za Msama Auction Mart za kukamata watu wanaowaibia wasanii.
"Sisi kama ASET tunaunga mkono juhudi za mkurufenzi wa Msama Auction Mart, Alex Msama na tuko tayari kumpa ushirikiano wa hali na mali ili aendelee kuwanasa wezi wa kazi za wasanii ambalo anaendelea nalo," alisema Asha.
Asha alisema kuwa kampuni yake imefungua milango wazi kwa Msama ili kumsaidia kifedha ama kumpa vijana wa kuzunguka nao kwenye msako wa kuwanasa wezi hao.
"Pia nina mpango wa kuwasiliana na baadhi ya wamiliki wa bendi ili tukutane na kuweka mkakati wa kuungana na Msama, kwani sisi wote ni waathirika wa hii hali, tunaibiwa kazi zetu na wajanja wachache," alisema.
Aliongeza kuwa bendi yake kwa sasa inaandaa albamu ya 11 hivyo hayuko tayari kuimba anaibiwa ambapo amewataka wadau wote wa muziki kuunga mkono juhudi za Msama kwa hali na mali ili kukomesha wizi huo.
Katika zoezi lake la kukamata wezi wa jkazi za wasanii, wiki iliyopita kampuni ya Msama Auction Mart ilikamata mitambo miwili ya kudurufu VCD za wasanii wa muziki wa Injili na wa dansi maeneo ya Mabibo na Kinondoni.
Katika hilo, walinasa pia VCD 164 tupu na nyingine 54 zilizokuwa zimesharekodiwa zikiandaliwa kupelekwa mitaani kwa ajili ya kuuzwa ambapo watuhumiwa walifikishwa kwenye vituo vya polisi vya Urafiki na Oysterbay.
Mendelezo wa zoezi la kunasa wezi wa kazi za wasanii, Msama Auction Mart ilishakamata VCD 1,108 zenye thamani ya Sh. milioni 20 na tayari watuhumiwa walishafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.
No comments:
Post a Comment