Bendi ya Extra Bongo leo itafanya onyesho maalum la kusikilizisha nyimbo zake za albamu ya pili 'Listening Part' mbele ya waandishi wa habari na wadau mbalimbali za muziki wa dansi.
Kiongozi wa bendi hiyo Rogert Hegga ameiambia Sugutiraha.blogspot kuwa onyesho hilo litafanyika leo Jumatano, Agosti 24 katika ukumbi wa Meeda Club Sinza- Mori, jijini Dar es Salaam.
Hegga alisema kuwa onyesho hilo linafanyika ikiwa ni siku chache baada ya bendi hiyo kumaliza kushuti video ya wimbo wa Watu na Falsafa uliotungwa na mwimbaji Banza Stone.
"Tulianza kwa video ya wimbo wa Mtenda Akitendewa ukafuatia huu wa Watu na Falsafa na sasa tunataka kuwaonyesha wadau wa muziki kile ambacho tumekifanya kwa kipindi chote cha Ramadhan," alisema.
Kiongozi huyo alifafanua kuwa nyimbo nyingine zilizobaki za 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Mashuu' na 'Bakutuka' zitainaingizwa kwenye video baada ya kumalizika sikukuu ya Idd.
Hegga alisema ana uhakika kuwa hatua ambayo bendi hiyo imefikia ya kujiimarisha ni kubwa kwa madai kwamba wapenzi wa muziki wa dansi wanazidi kuikubali kutokana na ubora wa muziki inaopiga.
Kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan, Extra Bongo inafanya onyesho moja kwa wiki ambalo hufanyika kila Jumamosi katika ukumbi wake wa nyumbani wa Meeda Club Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Aidha, Extra Bongo inajiandaa kutoa burudani siku ya Idd mosi katika ukumbi Meeda na kisha Idd pili itaibukia ndani ya ukumbi wa Wenge Garden uliopo Ukonga ili kuendelea kuwaburudisha wapenzi wa muziki wa dansi.
Bendi hiyo 'ilifufuka' upya ikiwa na albamu ya 'Mjini Mipango' ambayo nyimbo zake ni 'Laptop', 'First Lady', 'Maisha Taiti', 'Safari ya Maisha' na 'Wema' zilizochangia kuiweka kwenye chati.
No comments:
Post a Comment