Bendi ya Extra Bongo ambayo kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan inaendelea mazoezi ya nyimbo za albamu ya pili, imekamilisha kibao cha 'Bakutuka' kilichotungwa na kiongozi wa shoo wa bendi hiyo, Super Nyamwela.
Akizungumza na Sugutiraha.blogspot, Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki alisema kuwa kibao hicho kimekamilisha albamu ya pili ambayo itakuwa na nyimbo sita.
"Tulianza na wimbo wa Mtenda Akitendewa ukafuatia wa Fisadi wa Mapenzi, Watu na Falsafa, Neema, Mashuu na sasa tuna huu wa Bakutuka ambao umetungwa na kiongozi wetu wa shoo," alisema Choki.
Choki alisema, wimbo huo unaimbwa kwa lugha ya kiswahili na kuchanganywa kidogo na kimwera ambapo amefafanua kuwa 'Bakutuka' kwa lugha hiyo ya kimwera maana yake ni wanakimbia.
Hata hivyo hakuelezea zaidi wanaokimbia ni nani, lakini akaongeza kuwa ili kujua ujumbe uliomo katika kibao hicho ni kuusikiliza pale unapoimbwa na siyo kusimuliwa tu.
Mkurugenzi huyo alisema kibao hicho kitasikika kwa mara ya kwanza kesho Jumamosi kwenye onyesho la bendi hiyo katika ukumbi wa Meeda Club Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema juzi wanamuziki wake walikuwa na kazi ya kushuti video ya kibao cha 'Watu na Falsafa' kilichotungwa na Banza Stone huku wakitarajia kuendelea na vibao vingine wiki ijayo.
Alifafanua kuwa kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan bendi hiyo imekuwa ikifanya onyesho moja huku ikitumia muda mwingi kukamilisha albamu ya pili ambapo imesharekodi vibao vitano na kubakiza kimoja cha 'Bakutuka'.
No comments:
Post a Comment