Ikiwa ni siku chache tu baada ya kumchukua mnenguaji wa bendi ya Twanga Pepeta, Aisha Madinda, uongozi wa bendi ya Extra Bongo umesema unajiandaa kuongeza mwanamuziki mwingine mpya atakayechukuliwa siku yoyote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki aliiambia SUGUTIRAHA kuwa iko mbioni kuendelea kujiimarisha kwa kuongeza mwanamuziki mwingine kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa kimuziki.
Choki alisema kuwa huenda mwanamuziki huyo mpya akatambulishwa kwenye maonyesho ya vunja jungu ambayo yatafanyika kwenye kumbi za burudani za jijini Dar es Salaam.
"Tutakayemchukua atakuwa ni mwanamuziki wetu wa mwisho kuongezwa kwenye bendi ya Extra Bongo, lakini kwa sasa jina lake litaendelea kuwa siri li wabaya wetu wasije wakaingilia kati na kutuharibia," alisema.
Alisema, kitakachofanywa na Extra Bongo ni kuwashangaza wapenzi na wadau wa muziki wa dansi ni kumtambulisha mwanamuziki huyo kwenye maonyesho ya vunja jungu kama mambo yatakwenda kulingana na jinsi walivyopanga.
Alifafanua kuwa leo Jumatano bendi hiyo itaendelea na onyesho lake kama kawaida katika ukumbi wa Masai Bar na kufuatiwa na lingine kesho katika ukumbi wa Mzalendo Pub Makumbusho.
"Baada ya hapo yatafuatia maonyesho ya vunja jungu ambayo mwanamuziki wetu mpya anaweza kuwepo kuanzia Ijumaa katika ukumbi wa hoteli ya Vatican City, Sinza na kisha Jumamosi katika ukumbi wa Meeda," alisema.
Mkurugenzi huyo aliongeza kusema kuwa watakuwa na mwanamuziki wao huyo kwenye onyesho la Jumapili litakalofanyika kwa mara ya kwanza katika ukumbi wa Afri-Centre eneo la Msimbazi Ilala.
Extra Bongo ambayo inatamba na albamu ya kwanza ya 'Mjini Mipango', Extra Bongo pia inaandaa nyimbo za albamu ya pili ikiwa imekamilisha 'Mtenda Akitendewa', 'Watu na Falsafa', 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema' na 'Msinitenge'.
No comments:
Post a Comment