Bendi ya Extra Bongo 'Next Level' inatarajia kutumia kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili kukamilisha kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili huku ikifanya onyesho moja kwa wiki.
Kiongozi wa bendi hiyo Rogert Hegga ndiye aliyeliambia gazeti la NIPASHE wakati akizungumzia mikakati iliopo mbele ya Extra Bongo mara baada ya kuanza kwa mwezi huo Mtukufu.
Mbali na hilo, kiongozi huyo alisema Extra Bongo inatarajia kutumia kipindi hicho kuongeza 'kifaa' kimoja ambacho kitatambulishwa mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kukichukua.
"Tutakachokifanya ni usajili wa dirisha dogo kama ilivyo kwenye timu za soka, tunaongeza mwanamuziki mmoja tu na siwezi kumtaja kama ni mwimbaji mpiga chombo ila itajulikana wakati muafaka ukifika," alisema.
Alisema kuwa bendi hiyo sasa inajivunia mafanikio ambayo imeanza kuyapata ikiwa ni pamoja na kukubalika kwa mashabiki wa dansi wa ndani na nje ya jijini la Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alisema kuwa wiki chache zilizopita bendi hiyo ilifanya ziara kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro kwa ajili ya kujitambulisha kwa mashabiki wa dansi na kupokelewa kwa kishindo.
"Mashabiki wetu walijitokeza kwa wingi kutuunga mkono kwenye maonyesho yote ambayo tumefanya kwenye mikoa hiyo na ndivyo ilivyo hata jijini Dar es Salaam ambapo pia wamekuwa wakizidi kujitokeza kwa wingi," alisema Hegga.
Hegga alisema kuwa kwa sasa Extra Bongo imekalimisha nyimbo mpya za 'Watu na Falsafa', 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Nguvu na Akili', 'Mtenda Akitendewa' na 'Msinitenge' ambazo ni maandalizi ya albamu ya pili.
Aidha katika kutoa burudani, Hegga alisema kuwa leo Jumamosi bendi hiyo itafanya vitu vya ndani ya ukumbi wa Zakhem Mbagala na kesho itamalizia katika ukumbi wa mpya wa Chiluba uliopo Mabibo Mwisho.
No comments:
Post a Comment