Bendi ya Extra Bongo 'Next Level' inatarajia kutumia kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili kukamilisha kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki mara baada ya kumaliza ziara ya siku tatu ya utambulisho wa nyimbo mpya na wanamuziki wapya mkoani Morogoro.
Ziara hiyo ilifanyika wiki iliyopita baada ya kumaliza ile ya mikoa ya Lindi na Mtwara iliyofanyika hivi karibuni kwa mafanikio makubwa kutokana na kupata mashabiki wengi waliohudhuria maonyesho ya bendi hiyo.
"Tumefanikiwa kujitambulisha kwa kushindo kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro na sasa tunajiandaa kutumia kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili ya kukamilisha albamu yetu," alisema Choki.
Choki alisema kuwa kwa sasa Extra Bongo ina nyimbo mpya za Watu na Falsafa, Fisadi wa Mapenzi, Neema, Nguvu na Akili na Msinitenge ambazo husikika kwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema ana uhakika kwamba kipindi chote cha Ramadhan kitatosha bendi hiyo kukamilisha kila kitu na hatimaye kuibuka kwa kishindo ikiwa na vitu vipya.
Mbali na hilo, Choki alisema kuwa katika mkakati ya kujiimarisha zaidi, bendi hiyo imepata gari dogo aina Hiace kwa usafiri ambalo litakuwa linatumiwa na wanamuziki wake kwenda kwenye maonyesho na kurudi nyumbani.
"Tumeanza na gari hili dogo lakini kadri mambo yanavyokwenda ndivyo tutaangalia uwezekano wa kununua kubwa zaidi ambalo tutakuwa tunalitumia kwa safari za maonyesho kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini,"alisema.
Aidha katika kutoa burudani, leo Jumatano bendi hiyo inapatikana katika ukumbi wa Equator Grill, Mtoni kwa Aziz , kesho Alhamisi itakuwa katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Makumbusho.
Maonyesho hayo yatafuatiwa na lingine la Jumamosi katika ukumbi wa Dolphin, Kimara na kumalizia wikiendi Jumapili kwa kutoa burudani katika ukumbi wa Stereo uliopo Kinondoni.
No comments:
Post a Comment