Dotinata aula nchini Burundi
MSANII wa siku nyingi wa fani ya maigizo na filamu, Husna Posh 'Dotinata', amepeta mkataba nchini Burundi ambao unamruhusu kuuza kazi za wasanii mbalimbali wa filamu wa hapa Tanzania.
Akizungumza na gazeti la NIPASHE, jijini Dar es Salaam, msanii huyo alisema kuwa aliingia mkataba huo mwezi uliopita na kampuni ya Burundi Intertainment Association ya nchini humo.
"Ni mkataba endelevu ambao niliingia na kampuni mwezi Juni ambapo wateja wa nchi za Congo DR, Rwanda na Uganda watakuwa wanafika Bujumbura kununua kazi za wasanii wa filamu wa Tanzania," alisema.
Alifafanua kuwa yeye ndiye atakuwa ananunua filamu za wasanii wa hapa nchini na kuzipeleka Bujmbura ili zikauzwe huko, kwa madai kwamba filamu za Tanzania zina soko kubwa nchini Burundi na zile za jirani na nchi hiyo.
"Nilianza kwa kuleta wasanii watatu wa Burundi ambao ni Shanel, Excellent na Olga, walikuja kushiriki kwenye filamu yangu ya nne ya Chupa Nyeusi na sasa wamerudi kwao," alisema.
Aliwataja baadhi ya wasanii wa hapa nchini ambao wameshiriki kwenye filamu hiyo kuwa ni Irene Uyowa, Tino Muya, Patcho Mwamba, Riama na wengine wenye makubwa katika fani hiyo.
Alisema huo ulikuwa ni mwanzo wa kuanzisha urafiki ambapo yeye (Dotinata) alikwenda nchini Burundi na kupata mkataba wa kuuza kazi za wasanii filamu nchini humo na kwamba atahakikisha Tanzania inajulikana kwa fani hiyo.
Mbali na filamu ya 'Chupa Nyeusi', Dotinata alizitaja nyingine ambazo alishakamilisha kuwa ni 'Ndani ya Gunia', 'Sekeseke', 'Hila', Ulimwengu wa Wafu na nyingine ya sita ambayo bado haijapewa jina.
No comments:
Post a Comment