Mpiga kinanda wa bendi ya Akudo Impact 'Vijana wa Masauti', Andrew Sekidia ambaye kwa sasa yuko Umangani akifanya shughuli za muziki huko, anatarajia kurudi kwenye bendi hiyo mwishoni mwa mwezi huu.
Meneja Uhusiano Msaidizi wa bendi hiyo, Ramadhan Pesambili, alisema, Sekidia aliaga na kwenda Oman kufanya kazi ya muziki kwa mkataba wa miezi mitatu ambao sasa unakaribia kumalizika.
"Sekidia atarudi kundini mwishoni mwa mwezi huu kwani tayari tumeshawasiliana naye akathibitisha kuwa kufikia Julai mwishoni atakuwa amesharudi ili kuendelea na kazi kwenye bendi yake ya Akudo," alisema Pesambili.
Pesambili alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa kwamba wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa mwanamuziki huyo ameitosa Akudo na kukimbilia nje ya nchi kufanya kazi ya muziki wa dansi.
"Huyo ni mwanamuziki wetu aliondoka kwa kuaga uongozi wa bendi na tumemuomba kwamba arudi na kinanda kingine ili tuwe na viwili, kwa hiyo taarifa kwamba ameacha bendi hazina ukweli wowote," alisema.
Meneja Uhusiano huyo Msaidizi aliongeza kusema kuwa Sekidia ndiye anayesubuiriwa ili kupiga kinanda kwenye nyimbo za albamu ya pili ya 'History no Change' ambazo bendi hiyo imezikamilisha.
Alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Ubinafsi', 'Umefulia', 'Pongezi kwa Wanandoa', 'Umejificha Wapi' ambapo Sekidia ataingia studio kwa ajili ya kucharaza kinanda.
Bendi hiyo inayoongozwa na Christian Bella imekuwa ikitamba na albamu ya kwanza ya 'Impact' ambayo ilichangia kuipandisha chati kwa nyimbo kali ukiwemo wa 'Yako Wapi Mapenzi'.
No comments:
Post a Comment