RAPA wa bendi ya Mashujaa Musica, Yanick Noa 'Sauti ya Radi', amesema kuwa amekamilisha kibao kiitwacho 'Mahakama ya Mapenzi' ambacho kimekamilisha albamu ya pili inayoandaliwa na bendi hiyo.
Sauti ya Radi ambaye ni Makamu wa Rais wa bendi hiyo, alisema kuwa Mashujaa Musica imekuwa kwenye maandalizi ya albamu ya pili ambapo imekamilisha kwa wimbo wake wa 'Mahakama ya Mapenzi'.
Mbali na wimbo huo nina rapu nyingi ikiwemo ya Kikombe cha Babu Loliondo ambayo kwa kweli ni moto wa kuotea mbali na imekuwa ikipendwa na mashabiki wengi wa bendi yetu ya Mashujaa Musica," alisema.
Alisema kuwa wimbo wake umeunganishwa na nyingine za 'Lucia', 'Uchungu wa Moyo', 'Ulishawahi Kwenda kwa Mkweo', 'Hukumu ya Mnafiki' na 'Shukrani' ambazo sasa zimekuwa zikipigwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Alifafanua kuwa bendi hiyo inaandaa albamu ya pili huku ikiendelea kuuza ile ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' na kuongeza kuwa kamilika kwa nyimbo mpya hakuna maana kwamba bendi hiyo itazindua albamu ya pili mapema.
Mwaka jana bendi hiyo ilizindua albamu hiyo ya 'Safari Yenye Vikwazo' ambayo hadi sasa imeendelea kutambulisha kwenye kumbi mbalimbali za ndani na nje ya jijini Dar es Salaam.
Bendi hiyo pia imekuwa ikifanya maonyesho matano kwa wiki ikianzia Jumatano hadi Jumapili kwa ajili ya kutamhulisha albamu hiyo na kujiongezea mashabiki zaidi wanaofika kuishuhudia.
Alisema kuwa kila Jumatano bendi hiyo imekuwa ikipatikana katika ukumbi wa Max Bar na kisha kuzunguka katika kumbi mbalimbali ukiwemo wa Mashujaa Night Park, Vingunguti na Bwalo Maofisa wa Magereza Ukonga.
No comments:
Post a Comment