Bendi za Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na Twanga Pepeta, zinatarajiwa kufanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za kusaidia matibabu ya mwanamuziki mkongwe, Muhidin Ngurumo.
Onyesho hilo litafanyika Jumamosi hii ya Julai 23 katika ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ndivyo mratibu wa Hassan Rehan ameiambia SUGUTIRAHA.blogspot.
Hassan alisema sehemu ya fedha zitakazopatikana kwenye onyesho hilo la pamoja zitakabidhiwa kwa mzee Ngurumo ama familia yake ili zitumike kwa ajili ya matibabu yake.
"Tuna uhakika kwamba wadau wa muziki wa dansi watakumbuka ambavyo mkongwe huyo wa muziki nchini alivyolazwa mara kadhaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," alisema Rehan.
Mratibu huyo alisema kuwa kutokana na Gurumo kuendelea kuugua, bendi za Twanga Pepeta na Msondo Ngoma zimeamua kufanya onyesho la pamoja ili kuchangisha fedha za matibabu kwa mzee huyo.
"Kwa ujumla ni kwamba maandalizi ya onyesho hilo yamekamilika ambapo kwa upande wa Twanga Pepeta itatumia nafasi hiyo kutambulisha nyimbo za albamu mpya inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu," alisema.
Alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Kauli', 'Kiapo cha Mapenzi', 'Umenivika Umasikini', 'Mtoto wa Mwisho', 'Dunia Daraja' na 'Penzi la Shemeji' utunzi wake Mwinjuma Muumin 'Kocha wa Dunia'.
Alifafanua kuwa kutokana na kuguswa na afya ya Gurumo, Twanga Pepeta ameamua kufanya onyesho hilo kwa vile mchango wake ni mkubwa kwenye muziki wa dansi na ni mshauri wa karibu wa bendi ya Twanga.
Rehani amewaomba Watanzania na hasa wapenzi wa muziki wa dansi kujenga utamaduni wa kusaidiana kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kuchangia matibabu ya wanamuziki ambao kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi wamejikuta wakishindwa kukidhi mahitaji ya gharama za matibabu wanapoumwa.
No comments:
Post a Comment