Upitishaji wa mkataba wa kimataifa wa 189 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO ni kama ni 'rungu' kwa waajiri walio na wafanyakazi wa majumbani watakaokiuka sheria na mikataba ya kazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta nyingine.
Mkataba huo wa kuwatambua wafanyakazi hao ulipitishwa Juni 16 mwaka huu katika mkutano wa 100 wa ILO uliofanyika nchini Uswisi na siku moja kabla ya kupitishwa, Rais Jakaya Kikwete alihutubia mkutano huo kuuridhia.
Akizungumzia hatua hiyo, Mratibu wa Shirika la Wafanyakazi wa Majumbani kwa Kanda ya Afrika, IUF, Bi. Vicky Kanyoka, alisema kuridhiwa kwa mkataba huo kumetoa fursa na nafuu kwa watumishi hao wa majumbani.
Kanyoka, alisema kulingana na mkataba huo, wafanyakazi wa majumbani watatambuliwa kama wafanyakazi wengine, kulindwa na kupewa haki zao ikiwemo kusainishwa mikataba na makubaliano kabla ya kuanza kazi kwa muajiriwa.
Mratibu huyo alisema kitu cha muhimu baada ya kupitishwa kwa mkataba huo ni serikali ya Tanzania na wananchi wake kuutekeleza kwa vitendo ili wafanyakazi hao wanajivunie kazi yao tofauti na siku za nyuma walipokuwa wakijificha.
"Kwa hakika kupitishwa kwa mkataba huo wa 189 ni kama rungu kwa wafanyakazi wa majumbani, watawabana waajiri wao, ambao kwa miaka mingi waliwabagua, kuwanyanyasa na kuwadharau wakiwachukulia kama 'vijakazi'," alisema.
Aliwataka watumishi hao kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mkataba huo kwa kutokubali kuajiriwa kabla ya kuingia mkataba na kuridhia haki zao stahiki katika ajira ili inapotokea tatizo mbele ya safari iwe rahisi kusaidiwa.
Aliwataka pia waajiri kuridhia na kuutekeleza mkataba huo kwa kuamini watumishi hao ni kama sehemu ya familia zao na hivyo kuwapa huduma na stahiki zote kama mishahara kulingana na kima wanachokubaliana na kwa muda muafaka.
Mratibu huyo alisema mkataba huo ulipitishwa kwa kupigiwa kura 396 za ndio huku kura 16 zikiukataa miongoni mwa nchi zilizougomea ikiwa ni taifa la Uingereza, huku mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania na yale ya Amerika Kusini na Kaskazini yakiongoza kwa kuupitisha.
No comments:
Post a Comment