Bendi ya Mashujaa Musica ambayo sasa inaendelea kukamilisha albamu ya pili, imeongeza wanamuziki wawili kundini ili kuendelea kuimarisha safu yake ya upigaji vyombo.
Kwa mujibu wa rais wa bendi hiyo, Jado Field Force, wanamuziki hao ambao walijiunga na Mashujaa Musica wiki iliyopita ni Kassim Hamis anayepiga gita la besi na Tatoo ambaye anapiga drums.
Jado alisema kuwa mpiga besi huyo ametokea bendi ya Rufita Connection yenye maskani yake Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam wakati mpiga drums amechukuliwa toka bendi mpya ya Ngoma Musica.
Rais huyo alisema awali bendi hiyo haikuwa na mpango wa kuongeza wanamuziki wapya kwenye bendi hiyo, lakini hata hivyo alifafanua kuwa sasa hali inawaruhusu kujiimarisha zaidi.
"Mwanzoni mwa mwaka huu tuliongeza wanamuziki na wanenguaji tukasema kwamba tumefunga milango ya kuchukua wanamuziki wapya, lakini imebidi tuongeze hawa wawili kwa sababu hali inaruhusu," alisema.
Alisema, bendi hiyo imeongeza wanamuziki wapya wakati ikiwa imekamilisha nyimbo za albamu ya pili za 'Lucia', 'Uchungu wa Moyo', 'Ulishawahi Kwenda kwa Mkweo', 'Hukumu ya Mnafiki', 'Shukrani' na 'Mahakama ya Mapenzi'.
Aliongeza kuwa mwaka huu ni Mashujaa Musica kuwa matawi ya juu kwa madai kwamba wamejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kujiimarisha kila idara kwa kupata wanamuziki wa kutosha wanaojua kazi ya muziki.
"Mwaka jana tulizindua albamu ya kwanza ya 'Safari Yenye Vikwazo' ambayo hadi sasa imeendelea kuwepo sokoni wakati sisi tukiwa kwenye maandalizi ya albamu ya pili," alisema Jado.
No comments:
Post a Comment