Mwezi mmoja baada ya kujiunga na bendi ya Kalunde, mwimbaji wa siku nyingi, Bob Rudala amegfyatia kibao cha 'Ulinipendea Nini' ambacho sasa kinafanyiwa mazoezi na wanamuziki wa bendi hiyo.
Kiongozi wa bendi hiyo Junior Grengo aliliambia gazeti la NIPASHE jana kuwa kibao hicho kitakuwa ni cha nne kukamilishwa na bendi hiyo ambayo iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili.
"Tulianza kukamilisha nyimbo tatu za 'Masumbuko', 'Sisee' na 'Fungua' ambazo tumekuwa tukizipiga kwenye maonyesho yetu ya kila mwisho wa wiki na sasa tunamalizia huu wa Rudala," alisema Grengo.
Alisema, kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa bendi hiyo imekuwa kambini ikiandaa nyimbo za albamu ya pili ikiendelea na maonyesho ya mwisho wa wiki katika kumbi mbalimbali za burudani ambapo sasa ina nyimbo nne.
"Rudala amejiunga na bendi yetu akiwa na wimbo wa Ulinipendea Nini ambao sasa uko hatua za mwisho kukamilika, huenda wiki ijayo ukaanza kusikika kwenye maonyesho yetu," alisema.
Alifafanua kuwa bendi hiyo imelazimika kuweka kambi ya mazoezi huku ikiendelea na maonyesho ya mwisho wa wiki ili isipoteze wapenzi na mashabiki wake ambao wamezoea kuishuhudia ikiwaburudisha.
Alisema kuwa kila Ijumaa kama leo imekuwa ikitoa burudani katika ukumbi wa Triniti uliyopo Oysterbay na kisha Jumamosi wamekuwa wakifanya vitu vyoa katika ukumbi wa Joevic, Mbezi Beach.
Mbali na maonyesho, alisema kuwa Jumapili hufanya bonanza ndani ya ukumbi wa Girraffe Oceanic View uliyopo Mbezi Beach ambapo siku zilizobaki huwa kambini kwa ajili ya mazoezi ya nyimbo mpya.
Aidha, hatua ya kumchukua Bob Rudala kutoka bendi ya InAfrika imekuwa ikielezwa kuwa inalenga kuifanya Kalunde ijulikane kitaifa na kimataifa kwa vile ana uzoefu wa kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment