Waimbaji wawili wa kike wa bendi ya Kalunde, Mwapwani Yahaya na Sarafina Mshindo, wamechukuliwa kwa muda kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Bongo Star Search.
Meneja wa Kalunde, Deborah Nyangi ambaye ni mwimbaji pekee wa kike aliyebaki kwa sasa katika bendi hiyo, ameliambia gazeti la NIPASHE kuwa uongozi umewaruhusu waimbaji hao kushiriki mashindano hayo.
"Kila wanapokuwa na nafasi wamekuwa wakienda kama kawaida kwenye maonyesho kama kawaida huku wakiendelea na mashindano hayo ambayo yaliwafanya wajulikane hadi tukawachukua mwaka 2009," alisema.
Alisema kuwa waimbaji hao wamechukuliwa kwenye mashindano hayo wakati bendi yao ikiwa kwenye maandalizi ya nyimbo za albamu ya pili ambazo wameshiriki kikamilifu.
Alisema kuwa hatua ya uongozi wa bendi kuwaruhusu wanamuziki hao kwenda kwenye mashindano hayo inalenga kutambua mchango wa kampuni Benchmark Production ambayo iliibua vipaji vyao hadi wakachukuliwa na Kalunde.
"Bila Benchmark sisi Kalunde tusingewajua Mwapwani na Sarafina, hivyo tunaheshimu sana mchango wa kampuni hiyo kwenye sanaa na hasa ya muziki wa dansi na kizazi kipya," alisema Deborah.
Kalunde ambayo hivi karibu ilipata mwanamuziki mpya Bob Rudala, kwa zaido ya mwezi mmoja saa iko kwenye maandalizi ya albamu ya pili na tayari imekamilisha nyimbo nne mpya.
Nyimbo hizo ni 'Masumbuko', 'Sisee', 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini' ambao umetungwa na Bob Rudala aliyejiunga na bendi hiyo akitokea katika kundi la InAfrika ambayo imekuwa ikipiga muziki kwenye nchi mbalimbali.
Huku ikiendelea kuandaa nyimbo mpya, bendi hiyo pia imekuwa ikitoa burudani kila Ijumaa katika ukumbi wa Triniti Oysterbay, Jumamosi huwa Joevic Pub Mbezi Beach na Jumapili katika ukumbi wa Giraffe Hotel Mbezi Beach.
No comments:
Post a Comment