Baada ya kukamilisha utunzi wa nyimbo za albamu ya 11, bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta International', imeanza kazi ya kurekodi nyimbo hizo hatua hadi zote zinakamilisha kurekodiwa.
Mkurugenzi wa kampuni ya ASET inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka amesema kuwa albamu hiyo ambayo haijapewa jina inaundwa na nyimbo sita.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni 'Dunia Daraja', 'Mapenzi Hayana Kiapo','Kauli', 'Mtoto wa Mwisho', 'Penzi la Shemeji' na 'Talaka Harusini' ambazo sasa zinapigwa kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
"Wanamuziki wameshaanza kuingia studio ili kurekodi nyimbo hizi , lakini katika hizo upo mmoja ambao tulishaurekodi na Bozi Boziana," alisema Asha.
Aliutaja wimbo huo kuwa ni 'Mapenzi Hayana Kiapo' ambao mkongwe huyo wa muziki wa dansi barani Afrika ameshiriki kikamilifu na waimbaji wake wa wawili wa kike aliotua nao hapa nchini hivi karibuni.
"Tutaendelea kuangusha moja moja studio ili kuhakikisha kwamba zote zinarekodiwa, yote haya ni maandalizi ya uzinduzi wa albamu yetu ambayo tumepanga kuizindua kabla ya kumalizika mwaka huu," alisema.
Bendi hiyo ambayo sasa inajiita 'Wazee wa Kisigino', imekuwa na utaratibu wa kuzindua albamu kila mwaka ambapo sasa inajiandaa kufanya uzinduzi huo wa albamu ya 11.
Twanga Pepeta pia imekuwa ikifanya maonyesho matano kwa wiki ikianzia Jumatano ambapo huwa katika ukumbi wa Billicanas na kufuatiwa na lingine Alhamisi katika ukumbi wa Sun Cirro.
Kwa siku ya Ijumaa bendi hiyo imekuwa ikizunguka kwenye kumbi mbalimbali kulingana na maombi ya mashabiki wake na kisha Jumamosi katika ukumbi wao wa nyumbani wa Mango Garden Kinondoni.
Jumapili mchana Twanga Pepeta hufanya vitu vyake kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni kabla ya kumalizia wikiendi kwa kufanya onyesho usiku katika ukumbi wa TCC Club Chang'ombe.
No comments:
Post a Comment