Monday, July 25, 2011

Anania Ngoriga naye ajiunga na bendi ya Kalunde

Mwanamuziki wa siku nyingi Anania Ngoriga ambaye ni mlemavu asiyeona, amejiunga na bendi ya muziki wa dansi ya Kalunde yenye maskani yake Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Ngoriga alijiunga rasmi na Kalunde wiki iliyopita ambapo tayari ameshaanza kushiriki kwenye maonyesho ya bendi hiyo kwenye kumbi mbalimbali za burudani na kuonyesha makali yake.
Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo ndani ya Kalunde, kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala, alisema ana uhakika wa bendi yake kuingia kwenye muziki wa ushindani kwa vile inaundwa na wanamuziki wazoefu.
"Siyo kwamba ni wanamuziki wazoefu tu, kwa ujumla ni kwamba Kalundi inaundwa na wanamuziki wanaoujua muziki kwa hiyo tuna uhakika wa kupata soko la muziki la ndani na nje ya nchi," alisema Rudala.
Alisema kuwa karibu wanamuziki wote wa Kalunde wana uwezo wa kuimba na kupiga vyombo vya muziki na kwamba bendi zenye wanamuziki wa aina hiyo hapa nchini ni chache ikiwemo Kalunde.
"Mfano mzuri ni huyu Ngoriga ambaye anaimba na pia anajua kupiga gita la solo, rythm na bendi, hivyo tuna uhakika wa kufanya mambo makubwa kwenye muziki wa dansi," alisema.
Rudala alisema kuwa mwanamuziki huyo amejiunga na Kalunde wakati ikiwa kwenye maandalizi ya albamu mpya ikiwa imekamilisha nyimbo nne za 'Masumbuko', 'Sisee', 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini'.
Mbali na hilo, aliongeza kuwa Ngoriga amekuta waimbaji wawili wa bendi hiyo ambao ni Sarafina Mshindo na Mwapwani Yahaya wakiwa kwenye mashindano ya Bongo Star Search baada ya kufanikiwa kuingia 14 Bora.
"Furaha yetu imeongezeka zaidi, kwanza tulifurahi waimbaji wetu kuingia kwenye 14 Bora ya Bongo Star Search na sasa tumefurahi zaidi kwa kumpata mzoefu wa muziki wa dansi, Anania Ngoriga," alisema.
Naye Ngoriga mwenyewe alisema kuwa amejiunga na Kalunde akitokea katika bendi ya Karafuu ya visiwani Zanzibar ambayo alidumu nayo kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema, amejiunga na Kalunde kwa kutambua kuwa ni bendi yenye wanamuziki wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi ya muziki na kuongeza kuwa atashirikiana nao ili kuhakikisha kwamba inazidi kupiga hatua.

No comments:

Post a Comment