Sunday, July 31, 2011

Extra Bongo sasa kuwa na onyesho moja wakati huu wa mfungo wa Ramadhan.

Bendi ya Extra Bongo 'Wazee wa Kizigol', inatarajia kutumia kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kurekodi na kushuti video ya nyimbo za albamu ya pili huku ikifanya onyesho moja kwa wiki.
Hayo yalisemwa na meneja wa bendi hiyo, Mujibu Hamis wakati akizungumzia kile ambacho kitafanywa na Extra Bongo wakati wote wa mfungo huo ambao ulianza juzi.
Alisema, ingawa bendi hiyo imekuwa ikiombwa kwenda mikoa mbalimbali kutoa burudani, wanamuziki wameona ni bora kwanza wakamilisha albamu hiyo ili wawe na nyimbo za kutosha katika maonyesho yao.
"Ndivyo tulivyoamua kwamba wakati wa Ramadhan tuwe na onyesho moja tu kwa wiki ili siku nyingine tuzitumie katika kukamilisha nyimbo za albamu ya pili lakini akija mtu kutukodi tukwenda kumfanyia kazi," alisema Mujibu.
Meneja huyo alifafanua kuwa hilo onyesho moja kwa wiki litakuwa linafanyika kila Jumamosi katika ukumbi wa Meeda club uliopo Sinza-Mori, jijini Dar es Salaam.
Alisema, Extra Bongo imekalimisha baadhi ya nyimbo za albamu ya  pili zikiwemo za 'Fisadi wa Mapenzi, 'Watu na Falsafa', 'Fisadi wa Mapenzi', 'Neema', 'Nguvu na Akili', 'Mtenda Akitendewa' na 'Msinitenge'.
"Kwa ujumla ni kwamba tunataka tukamilishe albamu ya pili wakati wa mfungo wa Ramadhan, ndio maana tukajiwekea ratiba hiyo ya kufanya onyesho moja kwa wiki huku tukiendelea kurekodi na kushuti video," alisema.
Extra Bongo ilianza kwa albamu ya 'Mjini Mipango' ikiwa na nyimbo za 'Laptop', 'First Lady', 'Maisha Taiti', 'Safari ya Maisha' na  Wema ambazo zimekuwa 'zikiporomoshwa' kwenye maonyesho ya bendi hiyo.
Aidha, bendi hiyo kwa sasa imekuwa ikifanyia mazoezi baadhi ya nyimbo za zamani zikiwemo za 'Fadhila kwa Wazazi', 'Mwaka wa Tabu' na nyingine nyingi ambazo Ally Choki na Rogert Hegga waliwahi kutamba nazo.

No comments:

Post a Comment