Wednesday, July 6, 2011

Wajumbe wa nyumba 10 CCM nao wanataka kulipwa posho!

WAKATI sakata la kutaka posho za wabunge ziondolewe likiendelea kuwa gumzo miongoni mwa wananchi, wajumbe wa nyumba kumi wa CCM nao wameibuka na kutaka wawe walipwa posho hizo ili wanufaike nazo.
Kwa sasa sakata hilo limemalizwa bungeni baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutamka bungeni kuwa zitaendelea kutolewa licha ya baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani kutaka ziondelewe.
Hatua hiyo ya wabunge wa upinzani kutaka posho za kukaa bungeni ziondolewe na serikali ya kuamua ziendelee kuwepo imezua gmijadala miingi mitaani na kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni.
Sehemu kubwa ya wakazi wa Dar es salaam waliozungumza na gazeti hili walionyesha kutoridhishwa na kuendelea kuwepo kwa posho hizo huku wakitaka fedha zielekezwe kwenye matatizo yanayowakabili Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, wajumbe wa nyumba kumi wa CCM nao wameibuka na kutaka walipwe posho kama ambavyo madiwani na wabunge wanavyopata wanapokuwa kwenye vikao vyao.
Waliodai posho hizo ni wajumbe wa nyumba kumi wa kata ya Ndugumbi, jijini Dar es Salaam walipokuwa kwenye kikao kilichoitikishwa na diwani wa kata hiyo, Charles Mgonja ili kujadili utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Diwani huyo alielezea utekezaji wa ilani ya chama hicho ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwenye maeneo kadhaa ya kata yake na kwamba serikali inaendelea kutekeleza ilani ya CCM.
Baada ya hapo ndipo wajumbe wakapewa nafasi ya kuuliza maswali ama kutoa dukuduku zao ambapo walianza kuelezea uchafuzi wa mazingira na vibanda vya video ambavyo vindaiwa kuwaharibu watoto.
Aliyeanza kuchangia ni mjumbe wa shina namba 15 Kagera Mikoroshini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Mwenjala aliyedai kuwa kwenye eneo lake mkandarasi wa kuzoa taka amekuwa hafiki kwa wakati kuzoa taka.
Alisema hali hiyo inasababisha wananchi kulazimika kutupa taka kwenye mitaro hasa baada ya kuona mkandarasi haji kwa wakati ili kuzichukua na kuzipeleka kwenye dampo.
Wakati mjumbe huyo akisema hayo, mwingine aliyejitambulisha kwa jina la MagdalenaNguyeje wa shina namba 24, Kagera Kisiwani, alilalamikia vibanda vya video vilivyoko mitaani ambavyo sasa vinachangia kuwaharibu watoto.
Baada ya mjumbe huyo, aliibuka mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Mhangia wa shina namba 31, Kagera Kisiwani na kudai kuwa umefika wakati sasa wajumbe wa nyumba kumi nao wapete posho.
"Na sisi sasa tunastahili kupata posho kama ilivyo kwenu madiwani na wabunge, hivyo tunakuomba mheshimiwa diwani utusaidia kwa hilo, siyo posho ziishie huko juu tu, zishuke hadi kwetu huku," alisema Mhangia.
Ombi la mjumbe huyu liliunmgwa mkono na mwingine aliyejitambulishwa kwa jina la Hellena Muya wa shina la 10, Kagera Kisiwani aliyesema kuwa wao pia wanafanya kubwa, hivyo wanastahili kupata posho.
Akijibu maombi hayo, diwani huyo alisema suala la posho kiachiwe chama ngazi ya taifa kwa vile kinalijua na kwamba yeye hana uwezo wa kulitokea maamuzi na pia kwenye manispaa hakuna posho za wajumbe wa nyumba kumi.
Kuhusu kuwepo kwa vibanda vya video vinavyowaharibu watoto, aliwaomba wajumbe hao kushirikiana na viongozi wao wa serikali za mitaa ili kukomesha hali hiyo na kuhakikisha watoto wanakwenda shule badala ya kuishia vibandani.
"Suala na mkandarasi wa kuzoa taka kuchelewa nitafuatilia, lakini pia wananchi wahimizwe kulipia fedha za uzoaji taka na wala wasiendelee kutupa taka kwenye mitaro, huo ni uchafuzi wa mazingira," alisema Mgonja.

No comments:

Post a Comment